HOTUBA YA MGENI RASMI MH. MKUU WA MKOA WA DODOMA CAPT.
MSTAAFU CHIKU GALAWA YA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA SIKU 16 KUPINGA UKATILI NA
UNYANYASAJI WA KIJINSIA NA WATOTO MKOA WA DODOMA.
Awali ya yote napenda kutoa
shukurani zangu za dhati kwa kunialika na kunipa heshima ya kuwa mgeni Rasmi
katika hafla hii ya ufunguzi wa Siku 16 za Maadhimisho ya kupinga Ukatili na
Unyanyasaji wa Kijinsia na watoto katika Mkoa wetu wa Dodoma.
Pili natoa shukurani za
dhati kwa Washiriki wote na Kamati ya maandalizi kwa kazi nzuri mliyoifanya
pamoja na wadau wote mlioacha shughuli zenu kuungana na dunia nzima kupaza
sauti zenu na kutoa ujumbe wenu kwa watu wote Kupinga aina zote za Ukatili na
Unyanyasaji wa kijinsia na watoto.
Ndugu wananchi;
Sisi wana Dodoma
pamoja na Taifa letu tunaungana na dunia nzima kufanya maadhimisho ya siku 16
ya kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia ambayo huadhimishwa kila mwaka
kwa siku 16 kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba.
Kauli mbiu yetu ya
mwaka huu ni “FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU”. Kauli
mbiu hii inatujengea uwezo na ufahamu wa kina ya kwamba msingi wa mabadiliko
kitabia, makuzi bora ya watoto, ndoto njema, dira njema inaanza katika familia.
Mtoto akipata malezi bora na Elimu bora inamjengea uwezo wa kujitambua na
kuwa shujaa na kuwa na mwanzo ulio bora wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Ndugu wananchi;
Maadhimisho haya
yanatoa fursa kwa jamii kujifunza, kuelewa na kuchukua hatua dhidi ya vitendo
viovu vya Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia na watoto. Tunapofanya
maadhimisho haya kwa vitendo ni kupaza sauti zetu tunaojitambua kuwafichua
wahalifu wote na kuhakikisha kwamba familia zetu ni salama na zenye
ustawi bora. Wana Dodoma tutumie siku hizi 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji
wa Kijinsia na watoto kuleta mabadiliko ya kweli, kutambua aina zote za ukatili
katika familia zetu na kuchukua hatua kuzitokomeza.
Ndugu wananchi;
Tatizo la Ukatili na
Unyanyasaji wa Kijinsia lipo na linaendelea kuathiri watu wengi hasa wale walio
katika makundi maalum yanayoonewa kama Wanawake, Watoto, Walemavu na Wazee.
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vina athari nyingi kwa jamii zikiwemo athari za
Kiafya, Kijamii, Kiuchumi, Kisaikolojia na hata Kisiasa. Kupitia maadhimisho
haya naamini wananchi tutapata ufahamu wa kutosha kupitia midahalo, elimu kupitia
redio mbalimbali za hapa Dodoma, kuwatembelea watoto waishio kwenye mazingira
magumu, kukutana na watu wenye ulemavu na kutambua aina mbalimbali za Ukatili
na Unyanyasaji na kuchukua hatua zinazostahili pale yanapojitokeza.
Ndugu wananchi;
Watu waliofanyiwa
Ukatili wa aina yoyote huendelea kuwa wanyonge maisha yao yote na athari hizo
huwatesa maisha yao yote vizazi hadi vizazi. Mfano mzuri ni ongezeko la watoto
wanaoishi mitaani na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, watoto hawa
maisha yao hayawezi kuwa na furaha kwani hawatapati fursa za Elimu,
matibabu, malezi bora na mwisho wa maisha yao ni mateso. Wengine
huzama katika maisha hatarishi ya ukahaba, utumiaji madawa ya kulevya na
ujambazi hata vizazi vyao vinaendelea kurithi mateso hayo.
Ndugu wananchi;
Niwajibu wa kila mmoja
kulaani na kupinga vikali ukatili wa kijinsia, toa taarifa kwa vyombo husika na
Jeshi la Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka. Ifahamike kuwa jukumu la
kupambana na makosa ya ukatili wa kijinsia si la mtu mmoja, Asasi au Taasisi
fulani bali ni jukumu la Jamii nzima. Kila mtu aguswe katika nafsi yake
kutokomeza ukatili.
Vitendo vya Ukatili wa
kijinsia vinafanyika Majumbani mwetu ndani ya familia, mitaani na mahali popote
pale vyaweza kutokea. Vyanzo vya ukatili majumbani vinasababishwa na matumizi
ya pombe kupindukia, madawa ya kulevya, mila potofu na umasikini uliokithiri.
Moja ya watekelezaji wa ukatili huo yaweza kuwa mzazi mmoja au wazazi wote,
wanafamilia, majirani, makundi ya watu na waajiri wa wafanyakazi majumbani.
Ndugu wananchi;
Natambua kuwa kwa
nafasi na nyakati tofauti; Taasisi mbalimbali za Umma, Vyombo vya dola,
Mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za Dini na Afya wamekuwa wakifanya
jitihada nyingi katika kuhakikisha Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia unapungua
ili kuwa na jamii inayostawi vizuri. Juhudi hizi yafaa kuungwa mkono na watu
wote kwani jamii inapoharibika watu wote tusitegemee kuwa salama. Pia
Serikali inatambua na kuthamini michango ya wadau binafsi na tasisi zote
zinavyoshiriki kwa vitendo kupinga Ukatili na Unyanyasi wa Kijinsia na Watoto
kama tunavyoona mlivyoshirika hapa leo; tuendelee kuisaidia jamii kwa pamoja
kutokomeza unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia.
Ndugu wananchi;
Nimatarajio yangu
kwamba tunapofanya maadhimisho haya ya siku 16 tunataarajia kwamba jamii
itajitokeza bila woga kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa,
ustawi wa jamii na Polisi ili kufichua makosa ya Ukatili na
Unyanyasaji wa Kijinsia na Watoto. Aidha ni nipo taayari kupokea taarifa za
siri dhidi ya matukio haya,iwapo mtoa taarifa huyo ataona ana wasiwasi au bado
haamini mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya ngazi nilizozitaja na Jeshi
la Polisi. Naagiza watendaji waliyo chini yangu kufanya hivyo pale mtoa
taarifa za siri anapoomba msaada huo. Ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia ni
Uhalifu ambao kamwe haukubaliki. Matarajio yangu kuona kwamba ushughulikiaji wa
makosa haya unafanyika kwa Haki na hatua zinachukuliwa haraka kwa mujibu wa sheria
za nchi. Matokeo mazuri ya ushughulikiaji makosa ya aina hii yatakuza uelewa
kwa jamii kufichua uhalifu huo na hatimaye uhalifu wa aina hiyo kumalizika na
kuwa na Jamii bora isiyo na ukatili na unyanyasaji .
Ndugu wananchi;
Natoa wito pia kwa
Wanahabari kutumia kalamu zenu na kamera zenu kufichua popote walipo wahalifu
wa makosa haya. Wanaharakati wa Haki za Binadamu popote mlipo mpaze sauti
kupinga na kufichua matendo yote ya manyanyaso na ukatili wa Kijinsia na
Watoto. Natambua na nathamini mchango wa viongozi wetu wa dini, wahanga ni
waumiini wenu na hata wahalifu nao ni waumini wenu pia. Mkitukanya wote mtakuwa
mmetusadia kujenga Jamii Bora isiyokuwa na wanyanyasaji. Aidha Serikali
za Mitaa nazo zishiriki kikamilifu kwani ndiyo wapo karibu zaidi na wananchi.
Mwisho:
Kwa hotuba hii fupi
natamka kuwa NIMEFUNGUA RASMI maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili na
Unyanyasaji wa Kijinsia na watoto mkoani Dodoma.
“FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE
ELIMU”.
(ASANTENI KWA KUNISIKILIZA).
Tags
HABARI KITAIFA