Na Beatrice Lyimo- Maelezo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyataka Mabaraza na Bodi
za kitaalamu
za masuala ya afya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya
wataalam na vituo vinavyotoa huduma za afya kinyume cha Sheria.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo
alipokuwa akizindua Baraza la Optimetria, Baraza la wataalamu wa
Radiolojia pamoja na Bodi ya Maabara binafsi leo jijini Dar es salaam.
Alisema kisheria Mabaraza na Bodi
za Kitataalam ndivyo vyombo vinavyofuatilia ubora wa huduma za Afya
pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuwaepuka watoa huduma batili
wasiokuwa na utaalam na ujuzi wala kukidhi vigezo vya utoaji huduma
vilivyowekwa kisheria.
“Siku hizi kumekuwa na matumizi
makubwa ya vyeti vya kugushi vikiwemo vya vituo vya kutolea huduma na
wataalamu, watu wasio na taaluma wanatoa huduma kinyume na sheria hivyo
Mabaraza na Bodi mna mamlaka ya kuwachukulia hatua za kinidhamu,”
Alisema Waziri Ummy.
Aidha, alisema kuwa Serikali
haitasita kuyachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuvunja Bodi au
Mabaraza yatakayoshindwa kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika
sheria iliyohusika kuyaanzisha.
Aliyataka mabaraza hayo
kuhakikisha kuwa yanatoa Elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari
ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na ufahamu kuhusu huduma bora za afya
zitolewazo na wataalamu husika.
“Wananchi wakielimishwa wataepuka
watoa huduma batili wasiokuwa na utaalamu na ujuzi hivyo mabaraza na
Bodi vinapaswa kuhakikisha mambo haya hayatokei kwani vinauwezo mkubwa
wa kufuatilia masuala haya kwa mujibu wa Sheria”alifafanua Waziri Ummy.
Akizungumza kuhusu utendaji kazi
wa wataalamu hao Waziri Ummy amewataka wataalamu hao kujiendeleza
kielimu kwani utaalamu bila kuwa na ujuzi ni butu hivyo suala la elimu
lipewe kipaumbele.
Mbali na hayo Waziri ameitaka
Mabaraza na Bodi kuhakikisha wataalamu wote, vifaa na vitendanishi
vinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.
Tags
AFYA