……………………………………………………………………………………………………..
Hussein Makame-MAELEZO
Mahakama ya Tanzania imepiga hatua
kubwa kwa miaka mitatu iliyopita katika kusikiliza na kuamua mashauri
yaliyowasilishwa kwenye ngazi mbalimbali za mahakama nchini.
Hayo yamesemwa wakati Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipowaapisha
Jaji Shabani Ally Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Ferdinand
Wambali kuwa Jaji Kiongozi, Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza baada ya uapisho huo
Jaji Kiongozi, Wambali alibainisha mafanikio hayo ya mahakama na kuahidi
kuongeza kasi ya kutekeleza majukumu ya kusikiliza na kuamua mashauri
yanaypowasilishwa mahakamani.
Alisema moja ya kazi kubwa ya mahakama ni kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
“Hakuna shaka kwamba zipo
changamoto nyingi kuhusiana na uendeshaji wa mashauri lakini pia
tumepiga hatua kubwa kwa miaka mitatu iliyopita katika usikilizaji wa
mashauri” alisema Jaji Wambali na kuongeza:
“Kwa hiyo kasi ambayo imekuwa ipo
mimi naahidi kufanya kazi kwa bidii na nguvu zote kwa jinsi Mwenyezi
Mungu anavyonijalia kuhakikisha kwamba tunaendeleza pale ambapo wenzangu
wamafikia”.
Jaji Wambali alifafanua kuwa
mahakama inayo timu nzuri ya majaji na anaamini atashirikiana kwa dhati
na watumishi wengine kuhakikisha kwamba anatatua matatizo ya wananchi.
“Lakini kama mnavyofahamu mahakama
iko kwenye maboresho mengi na hasa kuhakikisha mahakama inakuwa karibu
na wananchi na mimi nitalisimamia hilo kwamba mahakama isiwe chombo
kinachoogopwa na wananchi bali kiwe chombo ambacho kinafikiwa na
wananchi kwa karibu” alieleza Jaji Wambali.
Alisema mambo manne ya msingi
aliyoyaapa ndiyo yatakamuongoza kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na
taratibu bila woga, upendeleo, chuki wala huba.
“Hayo ndio mambo makubwa manne
ambayo jaji yeyote yanamuongoza katika kutoa haki kwa hiyo hilo ndilo
linaloahidi kulitekeleza kwa nguvu zangu zote” alisema.
Akizungumzia kesi kukaa muda mrefu
bila kuamuliza, Jaji Wambali alisema sheria inataka kesi ya madai
isikae zaidi ya miaka miwili na mahakama imejipangia muda wa miezi 18 wa
kusikiliza kesi hizo, hata hivyo ameomba ushirikiano kwa wadau ili
kufanikisha lengo hilo.
“Ndio maana nimesema ni lazima
tushirikiano na wadau wote kwani wakati mwingine kesi zinaahirishwa kwa
sababu ya wadau.Lakini katika miaka hii miwili iliyopita sasa wananchi
wanatambua kwamba kesi zinaamuliwa kwa wingi sana kwa sababu kila Jaji,
hakimu amepangiwa kesi za kusikiliza kwa mwaka” alisema Jaji Wambali.
Alisema vipo vituo ambavyo
mahakimu na majaji wanamaliza kesi na wanatakiwa kwenda kwenye vituo
vingine kusaidia, hivyo watajitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba
wanalitekeleza hilo kwa nguvu zote.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama
ya Rufani,Jaji Shabani Ally Lila, alisema kuwa anakwenda Mahakama ya
Rufani kuongeza nguvu kwenye kusikiliza na kuamua mashauri.
“Najua Mahakama ya Rufani
inashughulika na kusikiliza na kuamua mashauri, kwa hiyo tutashirikiana
na wenzangu kuona namna ambavyo tutakabiliana na mashauri ambayo sasa
hivi yana muda mrefu mahakamani” alisema Jaji Lila.
Tags
HABARI KITAIFA