Makampuni ya ulinzi yanayofanya
shughuli zake Jijini Dar es Salaam yametakiwa kutoa mafunzo ya kila mara
kwa askari wake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na
changamoto za usalama zinazolikumba Jiji hilo kwa sasa.
Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa
Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni SACP Suzan Kaganda wakati
akifunga mafunzo ya siku tano kwa askari 70 wa kampuni ya ulinzi ya SGA
Security yaliyofayika katika makao makuu ya kampuni hiyo, Mbezi Beach.
Mafunzo haya yaliandaliwa na Polisi Tanzania katika kuimarisha ufanisi
wa askari katika makampuni binafsi.
“Natoa rai kwa makampuni mengine
ya ulinzi yaliyopo Mkoa wa Kinondoni yaige mfano mzuri kutoka SGA
Security kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wao ili kuwaongezea maarifa
yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kujiamini na kwa uhakika,” alisema.
Alisema jeshi la polisi liko
tayari kutoa ushirikiano, msaada wa kitaalamu na ushauri pale
itakapohitajika huku akiongeza kuwa jeshi hilo pekee haliwezi kumaliza
kabisa uhalifu bila kushirikiana na wadau mablimbali yakiwemo makampuni
kama SGA Security.
“Aidha nawaasa kuzingatia taratibu
na sheria za nchi tunapokuwa tukitimiza majukumu yetu ili kazi yetu iwe
na tija kwa jamii tunayoihudumia na taifa kwa ujumla,” alisema na
kuwaasa askari waliopata mafunzo kuyatumia vizuri kwa manufaa yao na
kampuni kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SGA
Security -Tanzania, Eric Sambu, alisema mafunzo hayo ya mara kwa mara
yamekuwa na manufaa makubwa kwa kampuni kwani wameweza kuwajengea askari
wao uwezo mkubwa hivi kuwafanya wananchi waongeze imani kwao. Zaidi,
Mkurungenzi Mtendaji alishukuru Polisi kuanzisha mchakato huu wa kutoa
mafunzo wao wenyewe moja kwa moja hii ni ishara kuwa kazi zetu katika
makampuni binafsi zinatambuliwa na Polisi wanatuchukulia kama wadau wao
katika kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
“Tumekuwa tukiendesha mafunzo haya
kwa kushirikiana na jeshi la polisi kwani kazi zetu zinafanana kwa kuwa
tupo ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,” alisema.
Alisema katika siku tano za
mafunzo askari hao waliweza kujifunza mada tofauti kama vile matumizi ya
nguvu na silaha za moto, haki za binadamu, polisi jamii, uvunjifu wa
haki za binadamu, huduma kwa wateja na uhusiano wa jamii, doria, eneo la
tukio, usuluhishi wa migogoro na nguvu ya kukamata.
“Tutaendelea kutoa mafunzo ya aina
hii mara kwa mara kwa kuwa tayari tumeona matunda yake ili askari wetu
kote nchini katika sehemu ambazo tunafanya kazi waendelee kuwa na uwezo
wa kufanya kazi kwa weledi,” alisema.
Kampuni ya SGA ni moja ya
makampuni makubwa ya ulinzi Afrika Mashariki huku ikiwa na uzoefu wa
zaidi ya miaka 40 katika ukanda huu na imeajiri zaidi ya wafanyakazi
17000 huku ikiwa imewekeza vikamilifu katika rasilimali tofauti za
shughuli za ulinzi na usalama.
SGA Security ni kampuni ya
kwanza binafsi kusajiliwa nchini Tanzania mwaka 1984, kama Group Four
Security baadae ikajulikana kama Security Group, baada ya zaidi ya miaka
32 ya shughuli na mafanikio Tanzania na 48 Afrika Mashariki, kampuni
imeweza mpaka sasa kuajiri wafanyakazi takriban 5,000 nchini Tanzania na
zaidi ya 18,500 katika kanda ya Afrika Mashariki, SGA Security ni moja
ya waajiri kubwa katika eneo hilo.
SGA Security ina uwakilishi wa
kiasi kikubwa sana katika kila eneo la huduma ya usimamizi na
usafirishaji wa pesa na vitu vyenye thamani na inatoa huduma hizi kwa
zaidi ya Mabenki na Taasisi za Fedha 55 katika eneo la Afrika Mashariki,
pia kwenye kutoa huduma za ulinzi kwa takribani mashirika 65 binafsi,
kidiplomasia na NGO sekta katika eneo hilo. SGA Security imejikita zaidi
pia katika ulinzi shirikishi kupitia teknolojia zaidi za kisasa kama
Closed Circuit TV na Access Control, huduma za radio, Tracking ya magari
na ufuatiliaji wa mizigo iwapo safarini (RFID).
Tags
POLISI