
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani hapa limesitisha huduma za
umeme katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira (Kiwira Coal mine) na
ofisi za Jeshi la Polisi mkoani hapa baada ya taasisi hizo kushindwa
kulipa madeni zinazodaiwa na shirika hilo.
Meneja wa Tanesco Mkoa Mbeya, Benedict Bahati amesema mgodi wa Kiwira
unadaiwa Sh1.3 bilioni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linadaiwa
Sh700 milioni.
Bahati amesema wamefikia hatua hiyo kwa sababu wadaiwa hao hawajaonyesha
nia ya kulipa madeni yao ambayo ni ya muda mrefu na hivyo
kulisababishia shirika hilo kushindwa kujiendesha kwa ufanisi.
“Taasisi za Serikali ambazo madeni yake ni makubwa na mwitikio wake
wa ulipaji sio mzuri, tumesitisha huduma mpaka watakapolipa madeni
hayo,”amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari amekiri kudaiwa
deni na Tanesco pamoja na kusitishiwa huduma hiyo kwenye baadhi ya
vitengo na kwamba wao kama taasisi wanadaiwa kama ilivyo kwa taasisi
nyingine.
Tags
Tanesco