Mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
BILIONEA kutoka Oman ameonyesha
nia ya kutaka kuwekeza Simba kwa kutaka kujitosa katika mchakato wa
kununua hisa za klabu hiyo ili awe sehemu ya umiliki wa timu hiyo kwa
asilimia 50.
Kutokana na hali hiyo, hali ya
mambo hivi sasa ndani ya Simba ni mshikemshike baada ya zoezi la
mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kuanza hivi
karibuni.
Mchakato wa bilionea huyo
kutia mguu katika kutaka kununua hisa hizo za kuimiliki Simba,
unafanyika kwa siri kubwa na hata kamati inayoshughulikia mabadiliko
hayo haiwezi kufahamu kwani bado haijakutana kuwajua walioweka nia.
Nia ya bilionea huyo wa Oman
kutaka kujitosa Simba, inaonekana kama kuleta upinzani kwa mwanachama
aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kununua hisa hizo mfanyabiashara
Mohamed Dewji ‘Mo’.
Mo yeye yupo tayari kutoa Sh
bilioni 20 lakini bilionea huyo wa Oman anaonekana kutaka kutoa kiasi
kikubwa cha fedha zaidi ya hizo anazotaka kutoa Mo.
Mchakato wa bilionea huyo
kutaka kununua hisa hizo unafanywa siri kubwa kwani hata baadhi ya watu
wa familia yake hawataki ijulikane kwa hivi sasa kwanza wakikataa
kuzungumzia mchakato mzima.
Bilionea huyo ambaye kwa sasa
jina lake tunalihifadhi anaonekana anataka mambo yake yaende kimyakimya
bila ya kutaka kujulikana kwanza, halafu baadaye ndipo awekwe wazi.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa
bilionea huyo alilikatalia gazeti hili kuhusu mpango huo wa ndugu yake
kutaka kununua hisa hizo za Simba lakini mmoja wa mabosi wa Simba
amethibitisha.
Bosi huyo alisema; “Kuna bilionea
mmoja ameonyesha kuwa na nia ya kutaka kununua hisa za kuimiliki Simba,
huyu mambo yake yanaenda kwa siri sana ili tuweze kufanikiwa.
“Huyo bilionea kutoka Oman
anamiliki visima vya mafuta pia ana uhusiano mzuri na klabu yetu kupitia
kwa kijana wake na yupo tayari kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 20 ambazo
Mo anataka kuwekeza.
“Hatuwezi kumtaja bilionea huyo
kwa sasa kwani tunahofia kuvuruga hali ya mambo wakati zoezi hili la
mabadiliko likiwa hatua za kwanza kabisa.”
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana
na hilo, Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna alisema: “Ni nani
aliyewaeleza taarifa hizo? Sina taarifa yoyote kuhusiana na watu hao.”
Mmoja wa watu wa kamati ya
mchakato wa mabadiliko hayo aliliambia Championi Jumamosi: “Ni ngumu
kujua kama huyo bilionea ameomba au la kwa maana, hizo tenda
hazijafunguliwa.
“Zitakapofunguliwa tutajua hayo
yote, ila mtu anaweza kuwa na nia halafu akamweleza mwenzake hiyo
inawezekana lakini kwetu kwa sasa hatuwezi kuwa na jibu la moja kwa
moja.”
Alipoulizwa kuhusu tetesi za
mfanyabiashara Said Salim Bakhresa kutaka kununua hisa hizo, alisema:
“Bakhresa hawezi kununua hisa za Simba kwani kanuni zinambana, yule
tayari ana timu ligi kuu na kanuni haziruhusu mmiliki mmoja kuwa na timu
mbili ligi kuu.”
Hata hivyo, bado nafasi kubwa ya
kumiliki hisa za Simba anapewa Mo ambaye ameonyesha kuwa bega kwa bega
na timu kwa muda mrefu, lakini kamati itakapofungua tenda lolote laweza
kutokea endapo kuna mtu ataweka fedha zaidi ya Sh bilioni 20 za Mo.
Tags
SIMBA SC
