NA MWANDISHI WETU, BUNDA
CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimesema
kitamchukulia fomu za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mwakani 2025 Dkt. Samia Suluhu Hasaan kutokana jinsi wanavyonufaika na uongozi
wake.
Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Mrida
Mshota Ameibainisha nia hiyo mbele ya waandishi wa Habari kijijini Sarakwa
wilayani Bunda mkoani Mara
Amesema kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia katika kuboresha sekta mbali mbali
za maendeleo nchini ikiwemo ufugaji, zimewashawishi wanachama wa chama hicho,
kumchukulia fomu za kuwania nafasi hiyo tena katika uchaguzi mkuu ujao.
"Miongoni mwa kundi lililonufaika sana na
uongozi wa Rais Samia ni sisi wafugaji; hivyo kwa kauli moja tumeazimia
kumchukulia fomu za kuwania nafasi hiyo mwakani ili kuonesha shukrani
zetu kwa mambo makubwa ya kimaendeleo aliyotutendea wafugaji kote
nchini," amesema.
Mshota amesema kuwa kwa muda wa miaka
mitatu tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 19,
2021 maisha ya wafugaji nchini yamekuwa bora zaidi kutokana na serikali
kuimarisha sekta ya mifugo kwa kuiwezesha katika maeneo ya pembejeo, malisho,
mikopo na masoko yenye tija.
"Kwa miaka mitatu ya Rais Samia madarakani
bajeti ya Wizara ya Mifugo imepanda kutoka Shilingi Bilioni 169 mpaka
Bilioni 460" amesema Mshota na kuongeza kwamba jumla ya wafugaji 8413
wamepatiwa mikopo mikubwa kutoka kwenye mabenki, iliyowasaidia kuboresha
shughuli za ufugaji kutoka ufugaji wa kimazoea hadi ufugaji wa kisasa.
Akizungumzia kuhusu pembejeo za mifugo amesema kuwa
kwa mwaka 2023/24 serikali imetoa lita 56,000 za dawa za kuoshea mifugo zenye
thamani ya shilingi bilioni 2.6 kwa wafugaji kote nchini.
Kuhusu wafugaji kumilikishwa ardhi, Mshota
amesema hekta milion 3.5 zimekwisha pimwa na kumilikishwa wafugaji maeneo
mbalimbali nchini, hatua iliyosaidia kupunguza migogoro baina yao na wakulima.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita katika
kuonesha inajali maslahi ya wafugaji nchini imechimba mabwawa 20 ya kunyweshea
mifugo sambamba na kuanzisha minada mipya ya mifugo 15 kote nchini.
Bosi huyo wa wafugaji pia amepongeza kuwa mpango wa
serikali wa kupitia Wizara ya Mifugo wa kutenga Shilingi bilioni 29 kwenye
bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kuchanja mifugo.