WAKATI Mwaka mpya wa masomo 2026 umeanza
leo Januari 13,2026 hapa kuna ujumbe kutoka kwa Mwalimu Doris Peter akianza kwa
kusema kuwa Huu si tu mwanzo wa vipindi vya darasani pekee, bali ni mwanzo wa
safari nyingine muhimu ya kujifunza, kukua na kujengwa kimaadili, kiakili, na
kiroho.
Katika safari hii, kila mhusika kwa maana ya Mwalimu, Mwanafunzi, Mzazi na jamii kwa ujumla wana nafasi ya kipekee ya kuwajibika mpaka kinachokusudiwa kiweze kutokea.
KWA MWALIMU:-
Mwalimu Doris anasema hiki ni kipindi
muhimu sana hasa kwa upande wa walimu ambao wamebeba dhamana ya kubeba vizazi
na kuibadilisha jamii, kiuelewa na kimaadili hivyo inabidi wawajibike kwa
uaminifu.
“walimu
Sisi ni taa katika giza la ujinga, tumebeba dhamana ya kubeba vizazi na kuibadilisha
jamii. Mwaka huu, na tuwajibike kwa uaminifu, kwa maombi na kwa upendo bila ubinafsi
wala upendeleo,
Tukumbuke kuwa tunafundisha zaidi kwa
maisha yetu kuliko kwa maneno. Tujitahidi kuwa mfano bora mbele za wanafunzi
wetu kwa nidhamu, kujituma, lugha njema na huruma”, anasema na kuongeza mwalimu
Doris.
Ameongeza kuwa, kila mwanafunzi ni mbegu
yenye uwezekano mkubwa wa kuota na kumea, “Hata yule mwenye changamoto, bado
anayo nafasi ya kuwa kitu kikubwa. Tusimkatae, bali tumkumbatie kwa huruma na
upendo”, amesema
KWA MWANAFUNZI:-
Aidha mwalimu Doris anasema kwa upande wa
Wanafunzi wanapaswa kuuanza mwaka huu kwa azma mpya, na kwamba wajitahidi kuzingatia
masomo, kuheshimu walimu, kuwa watiifu na mwenye bidii.
Ikumbukwe kuwa:- Mafanikio hayatoki kwenye
akili pekee, bali kwa nidhamu na maombi. Na kuwataka wasitazame changamoto za
nyumbani, familia au katika mazingira wanayotoka wala udhaifu walio nao, bali wamtazame Mungu aliye juu ya yote, na kwamba
Hakuna kinachoshindikana kwa Mungu, hivyo wajifunze kwa moyo wote, kwani elimu
ni silaha ambayo hakuna mtu anaweza kuiondoa.
“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote… Kumbukumbu la Torati 6:5-7” maana Mungu ndiye kila kitu katika vyote.
KWA WAZAZI:-
Pia Mwalimu Doris akawageukia Wazazi akiwataka
wawape Watoto wao ushirikiano wa kutosha na wa karibu katika kipindi chote wanapokuwa
masomoni.
“wazazi wapeni Watoto wenu ushikiano wa
kutosha, pamoja na kufuatilia maendeleo yao ya kimasomo, pia muwaombee, usiache
kamwe kuombea watoto wako tena omba kwa mzigo, wape muda, na waonyeshe upendo”,
amesema.
Amesema Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza na
kwamba Malezi bora huanzia nyumbani akiwataka wazazi kutenga muda wa
kuwasikiliza watoto, “mnapotoa mahitaji hakikisheni mnawalea Kiroho na Kimaadili
pia”,
Waleeni watoto kwa maombi na hekima. Huku
mkiendelea kushirikiana na walimu kwa karibu ili kuhakikisha mafanikio ya
watoto yanafikiwa kwa pamoja.
KWA JAMII KWA UJUMLA:-
Akizungumza na jamii Mwalimu Doris ameitaka
kujenga mazingira salama kwa watoto ili waweze kusoma na kukua kimaadili na
kiuelewa, ikiwa ni pamoja na kulinda ndoto zao.
“ Tuwe mstari wa mbele kuhimiza maadili
mema, kuchochea elimu na kuondoa vikwazo vya maendeleo yao tuhakikishe
tunalinda ndoto zao”, amesema.
Ameongeza kuwa ni vizuri “Tuupokee mwaka
wa masomo 2026 kwa maombi, kwa mipango, kwa bidii na kwa matumaini. Tumhusishe
Mungu katika kila hatua, tumkabidhi yeye majukumu yetu maana yeye ndiye muweza
na mfadhili wetu mkuu”, amesema mwalimu huyo mchangafu hasa anapokuwa kwenye
majukumu yake ya kazi.
KAULI MBIU YETU IWE:-
Kabla ya Kumaliza Mwalimu DORIS PETER anayefundisha
katika Shule ya Msingi ya Yusufu R makamba iliyopo Wilyani Temeke jijini Dar es
laam, anahanikiza kupitia Ukurasa wake wa Facebook kuwa ni vema Mwaka huu
kusimama na Mungu kwa ujasiri, na kwamba Kauli Mbiu ya 2026 iwe “Elimu kwa
maadili, na maadili kwa elimu.
"Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo
yako yatathibitika.”Mithali 16:3
Anamaliza kwa kusema “Mungu atupe neema
ya kusimamia wajibu wetu kwa uaminifu, na kutimiza kusudi lake katika maisha ya
kila mwanafunzi mwaka huu”,
KARIBU MWAKA MPYA WA MASOMO 2026
TUANZE KWA NEEMA, TUMALIZE KWA USHINDI.
MWISHO





