Hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtaja Kiongozi wa
Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi
jijini hapo kesho kuhojiwa, imewachefua baadhi ya wabunge.
Wabunge waliohojiwa mjini Dodoma jana, walisema kinachoendelea ni siasa badala ya uhalisia.
Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT – Wazalendo), Zitto Kabwe alisema
kinachoendelea ni siasa za kuchafuana na kwamba Makonda ajiandae kubeba
msalaba wake katika jambo hilo.
“Juzi hapa nililalamika bungeni kwamba leo wanakamatwa wasanii, kesho
watakamatwa wabunge. Mmeona leo Makonda amemtaja Mbowe. Kinachoendelea
ni siasa za kuchafuana. Kitendo cha Makonda kumtaja Mbowe maana yake ni
kwamba kazi anayoifanya si yake, ni kazi ambayo ametumwa na wakubwa wake
na ndiyo maana wanamuunga mkono,” alisema.
Zitto aliwataka wabunge wa upinzani bila kujali tofauti zao za vyama,
kuliona suala la Mbowe kuwa si shambulio kwa mbunge huyo wa Hai pekee
yake, bali ni mashambulizi dhidi ya wabunge wa upinzani. “Tukiliacha
bila kulisemea maana yake kesho na keshokutwa kila mbunge wa upinzani
anaweza kuonekana ni muuza dawa”.
Hata hivyo, Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu alisema anaamini
hadi Makonda kuamua kumtaja Mbowe na watu wengine, atakuwa na ushahidi
kwa sababu hawezi kufanya hivyo pasipo ushahidi. Balozi Adadi ambaye
aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alisema
anaamini kabla ya kutangaza majina hayo, aliwasiliana na Jeshi la Polisi
kwanza.
Lakini Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema wameamua
kumchukulia Makonda kama mtu anayetumwa, huku akisema Jeshi la Polisi
limemwachia mkuu huyo majukumu yake.
Tags
Bunge
