Wajumbe wa mkutano wa Mabadiliko
ya tabia ya nchi na athari zake kiuchumi hapa nchini uliokishirikisha
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini –Dodoma na Jumuiya ya Umoja wa
Ulaya (EU), wakiingia kwenye ukumbi wa Mikutano mmoja Jijini Dar es
salaam, siku ya kwanza ya mkutano huo wa Siku mbili.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa
Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina
(kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano uliohusu changamoto za
mabadiliko ya tabia ya nchi wakati wa mkutano uliowashirikisha wadau wa
maendeleo kutoka ndani nan je ya nchi na kuandaliwa na Chuo cha Mipango
ya Maendeleo Vijijini-Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo
akichangia mada mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi
yanavyoathiri uchumi wa wananchi vijijini nchini Tanzania,
zilizowasilishwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini-Dodoma, na kufanyika Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wadau wa mkutano
uliohusu changamoto za athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya
tabia ya nchi wakifuatilia kwa makini mjadala kuhusu suala hilo, Jijini
Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa
Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina
(kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi (kulia) wakiwa katika
picha ya pamoja nje ya ukumbi wa mkutano kuhusu Mabadiliko ya Tania
Nchi uliowashirikisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi uliofanyika
Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya
Maendeleo vijijini – Dodoma Dkt. Frank Hawassi akizungumza na wajumbe wa
Taasisi na Washirika wa Maendeleo kuhusu, umuhimu wa kuunganisha nguvu
katika kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi, katika Mkutano wa
Mabadiliko ya Tabia nchi jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa
Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina
akizungumza na wadau na Washirika wa Maendeleo kuhusu mradi wa Chololo
Ecovillage uliopo Dodoma unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) wakati wa
Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi jijini Dar es salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM).
………
Na Benny Mwaipaja,WFM
Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali
za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko
ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini
na katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi
na kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es
salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya
Maendeleo vijijini – Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano
uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha
Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa
kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo
hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais
inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili
kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia
nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za
kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la
Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini
na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya
wananchi”. Alifafanua Prof. Lokina
Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama Chololo Ecovillage unaofadhiliwa
na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma, ambao huwafundisha wanakijiji
njia bora za uzalishaji mali, hivyo kuwafanya baadhi ya Wananchi
waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza
kupata mazao ya kutosha na kuongeza pato lao.
Naye Mkuu wa Chuo hicho cha
Mipango ya Maendeleo vijijini- Dodoma, Dkt. Frank Hawassi, amezitaka
Taasisi na Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika
kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi
hazitachukuliwa athari zake zitampata kila mmoja.
Aidha, amesema hakuna nchi
inayoweza kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo bila kushirikiana hata
kama nchi hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia Jamii inapaswa kujua
kuwa hata matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine kuhusu ardhi ni
matokeo ya athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo kila mmoja
anatakiwa kuwa chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo
yanayopatikana yawe endelevu.
Ameongeza kuwa Chuo cha Mipango
Dodoma kinatoa nafasi kwa wadau kote nchini kukitumia kikamilifu katika
kutatua changamoto za kimazingira kwa kuwa ipo Idara iliyo na jukumu la
kushughulikia suala la Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi.
Kwa upande wake aliyekuwa Balozi
wa Umoja wa ulaya nchini Tanzania Tim Clarke, ambaye ameongoza timu ya
washirika wa Maendeleo katika Mkutano huo ameitaka Serikali kupitia
Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi kuwahamasisha wananchi kutumia
Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu
kwa kukata miti kwa ajili ya kupata Mkaa.
Vilevile ametoa rai kwa Serikali
kuwa karibu na jamii na kuwaelimisha kuhusu kutunza mazingira katika
shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato ili kusaidia kulinda
mazingira ya asili yatakayochochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja
na Taifa kwa ujumla.
Tags
UTAFITI