
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo
tarehe 30 Aprili 2017, ameungana na waumini wa dini ya Kikristo kusali
ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiaskofu, Jimbo Katoliki la Moshi
,Parokia ya Kristo Mfalme na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini mkoani
Kilimanjaro na kuwataka waumini wa makanisa hayo na Watanzania kwa
ujumla kuendeleza amani iliyopo nchini kwa kuwa ndio chachu ya
Maendeleo.
Rais Magufuli amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya Tano
zina lengo la kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli ya taifa
linalomuamini MUNGU.
'' Napenda muniamini kuwa mimi nipo kwa niaba yenu, najua huu Urais si
wangu, Urais mnao ninyi mlioamuwa nitumike kama mtumishi kwa wakati huu,
nawaomba sana muendelee kuniweka katika sala zenu ili kazi hii ya Urais
isinipe kiburi, nikawe mtumishi wa watu'' Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewashukuru waumini wa makanisa hayo mawili na watanzania
kwa ujumla kwa kusimama pamoja kuliombea Taifa amani iliyowezesha
wananchi kupiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na
kutokana na sala zao Mwenyezi MUNGU akamuwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli ametoa msaada wa mifuko 100 ya Saruji kusaidia
maendeleo ya kanisa Katoliki na Shilingi Milioni Moja kwa Kwaya ya
Kanisa hilo ili irekodi nyimbo zake, halikadhalka katika Kanisa la KKKT,
Mheshimiwa Rais ametoa mifuko 150 ya Saruji kwa ajili ya kuchangia
maendeleo ya Kanisa hilo na Shilingi milioni Moja kwa Kwaya ya Kanisa
hilo.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama amemuunga mkono Rais Magufuli kwa
Kuchangia Mifuko hamsini ya Saruji ambapo Mkuu wa Mkoa wa kilimanjaro
Mhe. Said Meck Sadick amechangia mifuko hamsini ya Saruji na Shilingi
laki Tano.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi ,Parokia ya Kristo
Mfalme Askofu Isaac Amani amemshukuru Rais Magufuli kwa uwamuzi wa
kusali kanisani hapo na kuwataka waumini wa kanisa hilo na Tanzania kwa
ujumla kuendelea kumuombea yeye pamoja na Serikali yake ili iweze
kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo na kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya mfano kwa Bara la Afrika.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania -
KKKT, Askofu Dr Fredrick Shoo amewataka waamini wa kanisa hilo na
watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu kwa mambo yanayofanywa na Rais
hususani katika kupambana na maovu, dhuluma na ufisadi vikiwemo na
badala yake Watanzania wabadilike na kujijengea mazoea ya kufanya kazi
halali na kuwa waaminifu na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Aidha, Askofu Shoo amemuomba Dkt Magufuli kuangalia uwezekano wa
kupunguza kodi hususani kwa taasisi za kidini zinzotoa huduma za kijamii
zikiwemo zile za Elimu na Afya.
Akijibu Maombi hayo Rais Dkt Magufuli amewaeleza waamini na watanzania
kwa ujumla kuwa Serikali inathamini michango ya huduma za kijamii
zinazotolewa na Taasisi za dini na kuahidi kuliangalia suala hilo.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Moshi, Kilimanjaro.
30 Aprili, 2017.
Tags
RAIS MAGUFULI