Kuhusu Mchezaji Abdi Banda Mechi
namba 194 (Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki wa Simba, Abdi Banda jezi
namba 24 amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la
kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla jezi namba 15
wakati akiwa hana mpira kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Alifanya kitendo hicho ambacho
hakikuonwa na waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 2, 2017
kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uamuzi wa Kamati umezingatia
Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda
alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na
Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar
iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda
kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na
Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kwa vile kosa hilo ni la
kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5)
wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya
Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika Klabu ya Simba
iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao
matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed
Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba
194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko
hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile
bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya
kufanya uamuzi.
Tags
MICHEZO KITAIFA