
Matukio ya utekaji watoto mjini Arusha yameanza kupata mwelekeo wa
ufumbuzi baada ya kijana wa miaka 18 kukiri kuwateka watoto wanne
alipokamatwa katika Mji wa Katoro wilayani Geita alikofanya tukio
jingine la utekaji.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari akiwa chini ya ulinzi wa polisi
jana, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Samson Petro alisema
watoto wawili aliwarudisha kwa wazazi wao baada ya kupewa Sh300,000.
Alisema wengine wawili aliwatelekeza mtaani baada ya wazazi wao kutotoa kiasi cha fedha walichotakiwa kumpa.
Samson alisema alianza ‘shughuli’ hiyo ya utekaji watoto kutokana na
mahitaji ya fedha na kwamba, aliacha shule akiwa kidato cha tatu katika
Shule ya Sekondari Lutozo iliyopo Katoro.
“Naishi na wazazi wangu, lakini nao ni masikini, nilifanya hivi ili
nipate fedha na nilikuwa nikimchukua mtoto naandika ujumbe kwenye
karatasi, naandika na namba ya simu napeleka karibu na familia ili
wanitafute,” alisema Samson.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema
walimkamata kijana huyo katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu
iliyopo mjini Katoro juzi saa mbili usiku.
Mwabulambo alisema polisi mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa
Arusha walifanya uchunguzi na kubaini mtuhumiwa alikuwa Katoro.
Alisema walipata taarifa za kutekwa Justin Ombeni (2) Septemba Mosi
nyumbani kwao katika eneo la Shilabela ambako mtuhumiwa alikwenda na
kuwakuta watoto wanne wakicheza nyuma ya nyumba.
Alisema aliwagawia pipi na kuondoka na Justin. Kamanda huyo alisema
polisi ilipata taarifa kuwa kijana huyo yupo chumba namba 103 katika
nyumba hiyo ya wageni ambako waliweka ulinzi kuizunguka.
Alisema walipoingia katika chumba hicho walimkuta akiwa na
mtoto huyo. Mwabulambo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Ombeni Mshana ambaye ni baba wa Justin alisema mtekaji huyo alimpatia
ujumbe mtoto wa jirani uliomtaka kutuma Sh4 milioni na walipokuwa
wakiwasiliana na mtuhumiwa alishusha kiwango hadi Sh1 milioni.
Alisema polisi walimtahadharisha kwamba asitume fedha hizo.Kamanda
Mwabulambo alisema tukio la kutekwa Justin ni la pili katika kipindi cha
miezi minne baada ya mwingine kutekwa.
Kesi kuhusu tukio hilo la kwanza inaendelea mahakamani baada ya mtoto kupatikana.
Katika hatua nyingine, kikosi kilichoundwa na wananchi mkoani Arusha
kikiongozwa na mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Kata ya Olasiti, Daudi
Safari na familia za watoto wawili waliotekwa kimewakamata watuhumiwa
wawili na kuwafikisha polisi.
Watoto hao ambao bado hawajapatikana ni Moureen David (6) anayesoma
darasa la kwanza shule ya msingi Lucky Vincent na Ikram Salim (3).
Wakizungumza jana nje ya kituo kikuu cha polisi Arusha baada ya
kuwafikisha kituoni watuhumiwa hao, Safari na wazazi wa watoto hao,
David Njau na Salim Kassim walisema kwa nyakati tofauti wameanzisha
msako baada ya
kuona siku zinakwenda bila watoto kupatikana.
Moureen alitekwa Agosti 21 saa 11 jioni akiwa anacheza nyumbani kwao
eneo la Olasiti, wakati Ikram alitekwa Agosti 26 saa 12 jioni akiwa
anacheza na watoto wenzake nyumbani kwao, Burka – Olasiti.
Safari alisema wamemkamata mtu mmoja (jina linahifadhiwa)
ambaye simu yake ilitumiwa na watekaji kuomba fedha kwa mzazi wa Ikram Salim.
Alisema pia wamemkamata wakala wa fedha wa kampuni moja ya simu (jina
tunaihifadhi) aliyetoa Sh300,000 kwa watekaji baada ya fedha kutumwa na
mzazi wa Ikram.
Imeelezwa kuwa wakala huyo amekamatwa kwa kuwa fedha hizo zilitolewa
pasipo kuorodheshwa popote na mpokeaji hakuonyesha kitambulisho
chochote.
Akizungumzia operesheni hiyo, Njau alisema hawatapumzika mpaka watoto wao wapatikane.
Alisema ufuatiliaji walioufanya kupitia minara ya kampuni za simu
unaonyesha wahusika walikuwa eneo la Kwa Mrombo jijini Arusha walipopiga
kuomba Sh4.5 milioni ili wamwachie Doreen na kiasi kingine kama hicho
kwa ajili ya Ikram.
Watekaji hao kupitia ujumbe waliotuma nyumbani kwa Njau walidai kama
wasipopewa fedha wangempoteza mtoto huyo japokuwa hawana nia hiyo.
Kassim Salim ambaye ni babu wa Ikram alisema, “tunaendelea kuomba msaada
zaidi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na vyombo vya dola
watusaidie tuwapate watoto wetu.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema juzi kuwa watu
watatu wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo akiwapo dereva wa
bodaboda mkazi wa Olasiti aliyetumwa kuwarejesha watoto wawili waliokuwa
wametekwa.
Matukio ya utekaji yalianza kuibuka Agosti 21 baada ya kutekwa watoto
wanne. Watoto wawili Ayoub Fred na Bakati Selemani wakazi wa eneo la
FFU, kata ya Murieti jirani na kata ya Olasiti walirejeshwa
Tags
watoto