Kituo cha kuthibiti magonjwa Afrika CDC chaibua wasiwasi kuhusu mikataba ya afya kati ya mataifa ya Afrika na Marekani
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa CDC, kimeibua wasiwasi juu ya makubaliano kati ya mataifa ya Afrika na Marekani kuhusu mikataba ya ufadhili katika sekta ya afya.
Kituo hicho kimesema, wasiwasi huo umetokana na mataifa ya Afrika kutakiwa kupeana data zake na taarifa za vimelea vinavyodhaniwa kusababisha milipuko ya magonjwa katika mataifa yao kama sharti la kupata ufadhili kutoka kwa serikali ya Marekani.
Mkurugenzi wa kituo hicho Jean Kaseya alisema awali alikuwa ameunga mkono mikakati hiyo kwa kuwa, ingewezesha nchi za Afrika kupata fedha moja kwa moja huku pia zikitakiwa kuwekeza kwa pamoja.
Lakini Kaseya alibainisha kuwa alikataa fursa ya kituo cha CDC kuwa mshiriki na mfuatiliaji wa makubaliano hayo, kwa sababu anaheshimu mamlaka ya kila taifa.
Hata hivyo, alisema kuwa shirika hilo limekuwa likiunga mkono mataifa mbalimbali pale linapohitajika kufanya hivyo na litaendelea kutoa ushauri endapo yatahitaji kujadiliana upya na Marekani, pamoja na kuzisaidia kutekeleza makubaliano yoyote yatakayotiwa saini.
Mataifa wanachama kupata usaidizi wa CDC
"Niliyaambia mataifa yote wanachama kwamba watapata usaidizi kamili kutoka CDC hata ikiwa masuala ya kujadili upya makubaliono yao," Kaseya alisema.
Siku ya Jumatano, Zimbabwe ilijiondoa kwenye mazungumzo na Marekani kuhusu makubaliano yake ya thamani ya dola milioni 367 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikieleza wasiwasi juu ya data zake ikisema kuwa makubaliano hayo hayakuwa ya usawa.
Serikali ya Zambia pia ilisema kuwa imepinga vipengee fulani vya makubaliano yake na serikali ya rais Donald Trump.
Wanaharakati wa masuala ya afya wamekosoa kipengele cha kupeana data muhimu kuhusu magonjwa kwa serikali ya Marekani kama sharti la kupata ufadhili wakihoji hatua hiyo,ni hatarishi kwa serikali za Afrika na raia wake.


