Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Muhammad Asif, anasema nchi yake imo kwenye vita vya wazi na Afghanistan.
Majira ya mchana baada ya sala ya Ijumaa (Februari 26), msemaji wa serikali ya Afghanistan, Zabihullah Mujahid, aliwaambia waandishi wa habari katika mji wa kusini wa Kandahar kwamba hata wakati yeye akiendesha mkutano huo, ndege za jeshi la Pakistan zilikuwa bado kwenye anga la Afghanistan.
Msemaji huyo ambaye awali baada ya mashambulizi ya asubuhi alikuwa amesema hakukuwa na taarifa yoyote ya watu waliouawa, alitowa taarifa mpya akitaja idadi ya vifo na majeruhi kwa mashambulizi ya alfajiri.
"Kufuatia mashambulizi yao, kwa mujibu wa idadi tuliyokusanya mpaka asubuhi hii, tuna mashahidi 13 mujahidina na majeruhi 22. Kwenye eneo moja, raia 13 walijeruhiwa pia. Ripoti za sasa ni kwamba huko Paktika, raia kadhaa pia wameuawa na kujeruhiwa, lakini idadi kamili bado haijathibitishwa," alisema.
Jeshi la Pakistan liliishambulia kwa makombora na mabomu miji kadhaa ya Afghanistan usiku wa kuamkia leo, yakiwa mashambulizi ya kwanza ya moja kwa moja dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Taliban, tangu washirika hao wa zamani walipogeukiana, kwa Islamad kuituhumu Kabul kuwahifadhi wanamgambo wanaofanya mashambulizi ndani ya ardhi yake.
Pakistan yadai kuwalenga wanajeshi wa Taliban
Vyanzo vya usalama ndani ya Pakistan vilisema mashambulizi hayo yalijumuisha makombora kutoka angani kwenye ofisi na vituo vya kijeshi vya Taliban katika miji ya Kabul, Kandahar na jimbo la Paktia, kujibu mashambulizi ya hapo jana yaliyofanywa na Afghanistan dhidi yake.
Taliban, ambayo inakanusha kuwahifadhi na kuwafadhili wanamgambo wa kundi la Taliban wa Kipakistan (TPP) na ina shutuma kama hizo dhidi ya jirani yake huyo, ilisema ilikuwa imefanya mashambulizi ya Alkhamis (Februari 26) kwa ajili tu ya kulipiza kisasi kwenye vituo vya kijeshi vya Pakistan mpaka mwao, lakini iko tayari kwa mazungumzo.
"Kwenye operesheni hiyo, wanajeshi 55 wa Pakistan waliuawa. Miongoni mwao, miili 23 ilichukuliwa na mujahidina kuletwa upande wetu. Wengine walikamatwa wakiwa hai, na idadi yao itatangazwa baadaye. Kuna pia idadi kubwa ya waliojeruhiwa. Kiasi kambi mbili za kijeshi na vituo 19 vya usalama viliharibiwa," alisema Zabihullah.
Juhudi za upatanishi
Duru kadhaa za mazungumzo kati ya Islamabad na Kabul zilifutia baada ya makubaliano ya awali ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Qatar, lakini juhudi zimeshindwa kuleta makubaliano ya kudumu.
Mwanajeshi wa Pakistan katika mpaka wa nchi yake na Afghanistan.Saudi Arabia iliingilia kati mwezi huu na kufanikiwa kuachiliwa kwa wanajeshi watatu wa Pakistan waliokamatwa nchini Afghanistan tangu Oktoba.
Iran, ambayo ina mpaka mkubwa wa mashariki na nchi zote mbili, imejitolea hivi leo kuwa mpatanishi, huku waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia akizungumza na wenzake wa Pakistan na China na kusema wanaendelea na juhudi za kukaa kitako na mahasimu hao huku wakiomba utulivu.

