
Kwa miaka mingi, kulikuwa na msemo uliokuwa ukivuma kwamba “Kigoma ni mwisho wa reli.” Ingawa ulitamkwa kwa utani, kwa kiasi kikubwa uliakisi hali halisi ya miundombinu na mtazamo uliokuwepo kuhusu mkoa huo. Wengi waliiona Kigoma kama eneo la mwisho wa safari badala ya lango la biashara na uchumi. Licha ya kuwa na Bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika na kupakana na masoko makubwa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Zambia, uwezo wake wa kuchochea biashara ya kikanda ulikuwa mdogo kutokana na changamoto za miundombinu ya usafirishaji. Gharama kubwa za kusafirisha mizigo, safari ndefu na kutokuwepo kwa mfumo wa kisasa wa uchukuzi vilifanya fursa nyingi za kiuchumi zibaki bila kutumika ipasavyo.
Hata hivyo, taswira hiyo inaanza kubadilika kupitia mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwekeza kwa wakati mmoja katika Reli ya Kisasa (SGR), bandari, usafiri wa majini, viwanja vya ndege na huduma nyingine za msingi. Badala ya kutekeleza miradi kama miradi ya kawaida ya maendeleo, Serikali imejenga mfumo jumuishi wa miundombinu unaolenga kuifanya Kigoma isiwe tena mwisho wa safari, bali lango la biashara, usafirishaji na uwekezaji litakalounganisha Tanzania na ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na Kusini mwa Afrika.
Mkakati huo unaendana na maono ya muda mrefu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka msisitizo katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa kama msingi wa kukuza uchumi shindani, kuongeza tija katika uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji barani Afrika. Dira hiyo inabainisha kuwa reli za kisasa, bandari, viwanja vya ndege, barabara na usafiri wa majini ni nguzo muhimu za kuunganisha masoko ya ndani na ya kikanda, kupunguza gharama za usafirishaji na kuvutia uwekezaji. Kwa muktadha huo, uwekezaji unaoendelea mkoani Kigoma haupaswi kutazamwa kama mradi wa maendeleo ya mkoa mmoja pekee, bali kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kujenga uchumi unaounganishwa na masoko ya Afrika Mashariki, ukanda wa Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anasema Kigoma haitakuwa tena mwisho wa reli bali mwanzo wa kufunguka kwa fursa za biashara na uwekezaji. Kauli hiyo inaonyesha mabadiliko makubwa ya namna Serikali inavyoutazama mkoa huo. Kwa mara ya kwanza, Kigoma inawekwa katika nafasi ya kuwa lango la biashara linalounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi za DRC, Burundi, Zambia pamoja na masoko mengine ya ukanda wa Maziwa Makuu. Reli ya kisasa itakapokamilika, bidhaa zitakazowasili Bandari ya Dar es Salaam zitasafirishwa kwa haraka hadi Kigoma na kuendelea kwa njia ya maji kwenda nchi jirani, hali itakayopunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa biashara ya Tanzania katika soko la kikanda.
Rais Dkt. Samia anasema Serikali inaendelea kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi unaounganisha reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini. Anafafanua kuwa mfumo huo utapunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ushindani wa biashara na kufungua masoko mapya kwa wafanyabiashara wa Tanzania. Maelekezo yake kwa Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na sekta binafsi kujenga karakana ya kisasa ya matengenezo ya meli mkoani Kigoma yanaonyesha kuwa Serikali haitaki mkoa huo ubaki kuwa eneo la kupitisha mizigo pekee, bali uwe kitovu cha huduma za kiufundi, ajira, uwekezaji na viwanda vinavyohusiana na sekta ya usafiri wa majini. Huu ni mkakati unaolenga kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha huduma za uchukuzi kwa ukanda mzima.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, anasema Serikali imeamua kuwekeza kwa wakati mmoja katika reli ya kisasa, bandari, usafiri wa majini na anga ili kujenga mfumo mmoja wa uchukuzi unaosaidiana. Kwa mtazamo wa kiuchumi, uwekezaji huo una maana kubwa kuliko kujenga miundombinu pekee. Reli itasafirisha mizigo kwa gharama nafuu kutoka maeneo ya uzalishaji hadi bandarini, meli zitaisafirisha kwenda nchi jirani kupitia Ziwa Tanganyika, huku viwanja vya ndege vikiongeza kasi ya usafiri wa watu na bidhaa zinazohitaji kufikishwa kwa haraka. Mfumo huo unatarajiwa kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha usafirishaji na ugavi kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.
Profesa Mbarawa anasema meli nne mpya za mizigo zitapunguza gharama za usafirishaji, kuongeza usalama wa safari katika Ziwa Tanganyika na kukuza biashara kati ya Tanzania, DRC na Burundi. Aidha, maboresho ya Bandari ya Kigoma pamoja na ujenzi wa gati jipya la mizigo na abiria yataongeza uwezo wa kupokea na kusafirisha mizigo kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Anaongeza kuwa Serikali imewekeza Shilingi bilioni 51.4 katika kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kigoma, jambo linaloonyesha kuwa mkakati wa maendeleo ya mkoa huo umejengwa kwa kuunganisha sekta zote muhimu za uchukuzi ili kuongeza mvuto wa uwekezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, anasema mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma utagharimu takribani Shilingi trilioni 6.3 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 48. Ujenzi huo unahusisha kilometa 411 za reli kuu, kilometa 95 za njia za kupishana, madaraja makubwa 27, madaraja madogo 75 pamoja na box culverts 475. Hizi si takwimu za kawaida za mradi wa ujenzi, bali zinaonyesha ukubwa wa uwekezaji ambao Serikali imeamua kuufanya ili kubadili kabisa mazingira ya biashara katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania.
Mhandisi Shiwa anasema treni za abiria zitakuwa na uwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa huku treni za mizigo zikikimbia kilometa 120 kwa saa. Anaeleza kuwa muda wa kusafirisha bidhaa kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam utapungua kwa kiwango kikubwa, hali itakayopunguza gharama za biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa katika Mkoa wa Kigoma na maeneo jirani. Aidha, Stesheni ya Kigoma kuwa ya nne kwa ukubwa nchini baada ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza ni ishara kuwa Serikali imekusudia kuifanya Kigoma kuwa kituo kikubwa cha biashara na usafirishaji kwa miaka mingi ijayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, anasema mafanikio ya miundombinu hayaishii kwenye reli na bandari pekee. Anasema vijiji vyote 363 vya Mkoa wa Kigoma tayari vimepata huduma ya umeme huku zaidi ya asilimia 75 ya vitongoji vikifikishiwa umeme. Anaongeza kuwa biashara kupitia mipaka ya Kobero na Manyovu imeongezeka kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, jambo linalothibitisha kuwa hata kabla ya kukamilika kwa SGR, Kigoma tayari imeanza kunufaika na nafasi yake ya kijiografia. Kwa mtazamo wake, reli mpya na meli za mizigo zitakuwa chachu ya kuongeza zaidi biashara hiyo na kuinua pato la Mkoa wa Kigoma pamoja na Taifa kwa ujumla.
Sirro anasema Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa kahawa, mahindi, maharage, mihogo, tangawizi, parachichi na mazao mengine ya biashara. Anaeleza kuwa kupatikana kwa reli ya kisasa na usafiri wa uhakika wa majini kutawapa wakulima uwezo wa kufikisha mazao yao kwenye masoko makubwa kwa haraka zaidi na kwa gharama ndogo. Aidha, sekta ya uvuvi itanufaika kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa kusafirisha samaki na bidhaa nyingine za uvuvi kwenda ndani na nje ya nchi. Kwa maoni yake, maendeleo ya miundombinu ndiyo msingi wa kuongeza thamani ya uzalishaji wa Kigoma na kuifanya iwe lango muhimu la biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Baba Levo, anasema wananchi wa Kigoma wanaona kwa macho yao mabadiliko yanayoletwa na Serikali kupitia uwekezaji katika maji, umeme, barabara, bandari na sasa Reli ya Kisasa. Anasema miradi hiyo imeanza kubadilisha maisha ya wananchi na kwamba mradi wa SGR utaendelea kukumbukwa na vizazi vijavyo kwa sababu umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya Mkoa wa Kigoma. Kwa mtazamo wake, miradi hiyo si ahadi za kisiasa bali ni uwekezaji unaobadilisha uchumi wa wananchi, unaovutia wawekezaji na kuongeza heshima ya Mkoa wa Kigoma katika ramani ya maendeleo ya Taifa.
Wafanyabiashara wa samaki katika soko la Kibirizi kwenye Manispaa ya Kigoma Ujiji, Amina Sadiki anasema uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo pamoja na kuendelea kuboreshwa kwa huduma za MV Liemba ni habari njema kwa wananchi wanaotegemea Ziwa Tanganyika kujipatia kipato. Anasema kwa muda mrefu wafanyabiashara walikuwa wakikabiliwa na gharama kubwa na changamoto za usafirishaji wa bidhaa kwenda Burundi na DRC, lakini sasa wanaamini meli hizo zitaongeza safari, kupunguza gharama na kufungua masoko mapya ya samaki na bidhaa nyingine. Kwa maoni yake, Kigoma inaanza kuchukua nafasi yake halisi kama lango la biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Naye mfanyabiashara wa mazao kutoka Uvinza, Adam Kalumanzila, anasema ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma ni ukombozi wa kweli kwa uchumi wa Mkoa wa Kigoma. Anaeleza kuwa gharama za kusafirisha mazao kwenda Dar es Salaam zimekuwa zikiwapunguzia faida wakulima na wafanyabiashara kwa miaka mingi, lakini SGR itabadilisha hali hiyo kwa kupunguza muda na gharama za usafirishaji. Anaamini mradi huo utavutia wawekezaji, kuongeza ajira kwa vijana, kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao na kuifanya Kigoma kuwa miongoni mwa mikoa yenye ukuaji mkubwa wa uchumi nchini.
Kwa ujumla, uwekezaji unaoendelea mkoani Kigoma unaonyesha kuwa Serikali imechagua kutumia miundombinu kama nyenzo ya kufungua uchumi wa mkoa huo na kuupanua zaidi katika ukanda wa Maziwa Makuu. Reli ya Kisasa, Bandari ya Kigoma, meli mpya za mizigo, maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Kigoma pamoja na upanuzi wa huduma za umeme na barabara ni sehemu za mfumo mmoja unaolenga kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo, kupunguza gharama za biashara na kuvutia uwekezaji.
Ndiyo maana kauli ya Rais Dkt. Samia kwamba “Kigoma haitakuwa tena mwisho wa reli bali mwanzo wa fursa za biashara na uwekezaji” haipaswi kutazamwa kama kauli ya kisiasa pekee, bali kama dira ya mabadiliko ya kiuchumi yanayolenga kuifanya Kigoma kuwa lango kuu la biashara, usafirishaji na uwekezaji linalounganisha Tanzania na ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na Kusini mwa Afrika.