BANDA MEDIA BLOG

SENYAMULE AHIMIZA USHIRIKIANO NA UADILIFU KULINDA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO


 Dodoma, Julai 21, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema ushirikiano, uwajibikaji na uadilifu ni msingi muhimu wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inaleta matokeo yaliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi.

Akifungua warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa wadau wa usimamizi wa miradi ya maendeleo, Julai 21, 2026, Mhe. Senyamule alisema warsha hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ushirikiano kati ya TAKUKURU na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi na kwa manufaa ya wananchi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta mbalimbali za maendeleo ili kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi.

“Sehemu kubwa ya bajeti ya Serikali inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kwa kuwa ndiyo chachu ya ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na nyinginezo. Hivyo ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha fedha za Umma zinasimamiwa kwa uwazi, ufanisi na uadilifu ili miradi ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa,” alisema Mhe. Senyamule.

Alisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa miradi unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, TAKUKURU, viongozi na wananchi ili kuziba mianya ya ubadhirifu na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa miradi.

Aidha, aliwataka washiriki wa warsha kutumia maarifa watakayopata kuimarisha ufuatiliaji wa miradi katika maeneo yao, kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua stahiki ili kuzuia kujirudia kwa mapungufu yaliyowahi kujitokeza.

Alieleza kuwa utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia viwango vya ubora, thamani halisi ya fedha na muda uliopangwa utaongeza imani ya wananchi kwa Serikali na kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Senyamule pia aliwahimiza wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uadilifu bila kusubiri kusukumwa, akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kulinda rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Christopher Mayans, alisema Serikali imeendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo mafanikio ya uwekezaji huo yanategemea usimamizi madhubuti kuanzia hatua ya upangaji, uidhinishaji, utekelezaji, usimamizi wa mikataba hadi kukamilika kwa miradi.

Aliongeza kuwa TAKUKURU inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika miradi ya maendeleo kwa lengo la kubaini mapema changamoto na kasoro zinazoweza kuathiri uwazi, ufanisi na thamani ya fedha za umma.     

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG