● Treni ya Mizigo Yafika Bahi
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa rai kwa wadau wa usafirishaji wa mizigo kutumia Reli ya Kisasa (SGR) ili kupunguza gharama za usafirishaji na kusafirisha mizigo kwa haraka na salama.
Mhandisi wa mradi huo kipande cha pili kutoka Morogoro mpaka Makutupora, Christina Samuel ametoa rai hiyo Julai 18, 2026 Bahi, mkoani Dodoma wakati wa ziara ya Waandishi wa Habari iliyoandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya mradi huo ikiwa ni matukio kuelekea katika uzinduzi na uwekaji Jiwe la Msingi wa Reli ya SGR, TABORA - KIGOMA utakayofanyika Julai 20, 2026 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Christina amesema kuwa, kutoka jijini Dar es Salaam hadi Makutupora kuna jumla ya stesheni tano za mizigo na nane za abiria huku stesheni ya Bahi ikiwa ni ya nne ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98.76 na imeshaanza kufanya kazi ya kusafirisha mizigo kati ya jijini Dar es Salaam na Bahi tangu mwezi Juni, 2026.
“Tunatoa rai kwa wadau wanaosafirisha mizigo kutumia usafiri wa SGR ili kupunguza muda wa safari kwani usafiri kati ya Bahi na Dar es Salaam unatumia masaa matano tu tofauti na barabarani ambapo yanaweza kutumika zaidi ya masaa 10 hadi 12, pia usafiri wa SGR ni nafuu zaidi na ni salama kama unavyoona hapa kuna kamera za kutosha na walinzi”, amesema Mhandisi Christina.
Mhandisi Christrina amefafanua kuwa kwa stesheni ya Bahi, treni inasafirisha mabehewa 10 ambapo kila behewa linabeba kontena mbili na kila kontena linabeba tani 28 huku eneo zima la mradi likiwa na uwezo wa kuhifadhi makontena mpaka 1,500.
Makontena hayo yanapofikishwa katika stesheni hiyo yanahamishiwa kwenye reli ya zamani na kupelekwa mpaka Kigoma, Isaka na Mwanza.
Aidha, ameeleza faida mbalimbali zinazotokana na mradi huo ikiwemo ongezeko la fursa za ajira, kuchochea ufanisi wa biashara kutokana na kupunguza muda wa safari pamoja na gharama za usafirishaji. Vile vile kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa kuwa mizigo inasafirishwa kwa njia ya reli.


