Dodoma, Julai 21, 2026 – Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, hatua ambayo imeongeza mvuto kwa wawekezaji wa sekta ya hoteli na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, wakati wa kikao chake na wamiliki wa hoteli Jijini Dodoma kilichofanyika Julai 20, 2026 katika Ukumbi wa Royal Village. Kikao hicho kililenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji hao ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Senyamule alisema maendeleo makubwa yanayoendelea kutekelezwa Dodoma yameifanya Mkoa huo kuwa kitovu cha uwekezaji na biashara.
> “Rais ameendelea kuimarisha Mkoa wa Dodoma na kuvutia wawekezaji wengi ambao wameona fursa zilizopo hapa. Wameamua kuwekeza kwa sababu wanaona maendeleo yanayoendelea yanaifanya Dodoma kuwa eneo lenye faida kibiashara na lenye uwezo wa kurejesha mitaji yao,” alisema
Mhe. Senyamule alibainisha kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, unaotarajiwa kuanza kutoa huduma baadaye mwaka huu, kutaongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi pamoja na mikutano ya kimataifa, hali itakayoongeza mahitaji ya huduma za malazi, hususan hoteli zenye hadhi ya nyota tano.
Aidha, alisema Mkoa wa Dodoma unaendelea kutekeleza mkakati wa kuufanya kuwa lango la watalii wanaokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, jambo litakaloongeza idadi ya wageni wanaokaa na kutumia huduma mbalimbali za hoteli na ukarimu ndani ya Mkoa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Hoteli Jijini Dodoma, Bw. Gabriel Maunda, alisema wawekezaji wa sekta hiyo wanaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akitoa rai kwa taasisi hizo kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ili kuondoa changamoto zinazoweza kuathiri mazingira ya biashara na uwekezaji.

