Farida Mangube Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo, amesema walimu wana nafasi ya kipekee katika maendeleo ya taifa kwani kila mtu duniani amepitia mikononi mwa mwalimu, hivyo wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha na kujitengenezea fursa za kiuchumi.
Prof. Nombo ametoa kauli hiyo mjini Morogoro alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa walimu wapya wa somo la Biashara watakaofundisha katika shule za sekondari za serikali nchini.
Amesema maboresho ya sera ya elimu na mitaala yaliyokamilika mwaka 2023 yanalenga kuhakikisha elimu inazalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine kupitia maarifa na ujuzi wanaoupata shuleni.
“Jukumu la mwalimu si kumfundisha mwanafunzi kufaulu mtihani pekee, bali kumwezesha kutatua changamoto zinazomzunguka kwa kutumia mazingira yake na kubadili elimu yake kuwa kipato. Awe amesoma Chemistry, Biology au somo lolote, lazima elimu yake imsaidie kuboresha maisha yake,” alisema Prof. Nombo
Alieleza kuwa katika maboresho hayo, serikali imeanzisha mikondo miwili ya elimu ambayo ni elimu ya jumla na elimu ya amali, huku somo la Biashara likiwa la lazima katika mikondo yote miwili kutokana na mchango wake katika kukuza ujasiriamali na stadi za maisha.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutekeleza mabadiliko hayo ya mitaala kwa ufanisi na kuwawezesha wanafunzi kutumia elimu yao kujenga uchumi wao binafsi na wa taifa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na shirika la Educate inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu ili kuongeza ubora wa ufundishaji wa somo la Biashara.
Amesema katika awamu hiyo walimu wapya 702 wamepatiwa mafunzo ya siku tatu yatakayowawezesha kufundisha somo la Biashara kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za sekondari za serikali.
“Mafunzo haya yanawajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji, kuandaa maandalizi ya kazi na kutekeleza mitaala mipya kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Dkt.Komba.
Aliongeza kuwa lengo kuu ni kuimarisha mbinu za kufundisha na kujifunza ili wanafunzi wahitimu wakiwa na ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiri wengine.
Dkt.Komba amesema tayari TET imeshatoa mafunzo kama hayo kwa walimu zaidi ya 1,500, huku awamu nyingine ikitarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti kwa walimu wa kujitolea watakaosaidia kufundisha somo la Biashara katika shule mbalimbali za serikali.
Amewataka wakurugenzi wa halmashauri na walimu kuwapa ushirikiano na usimamizi wa karibu walimu wa kujitolea ili kuhakikisha ufundishaji wa somo la Biashara unafanyika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

