BANDA MEDIA BLOG

WAZIRI MAVUNDE AELEKEZA USIMAMIZI THABITI WA SHERIA, ASILIMIA 90 YA BIDHAA NA HUDUMA MIGODINI ZITOLEWE NA WATANZANIA

 

Na Baltazar Mashaka, Mwanza

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameelekeza usimamizi madhubuti wa Sheria ya Madini na kanuni zake ili kuhakikisha asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi nchini zinazalishwa na kutolewa na Watanzania.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini, kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Mavunde ametoa maelekezo hayo Julai 22, 2026, wakati akizindua Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini lililofanyika jijini Mwanza.

Jukwaa hilo limewakutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma migodini, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi pamoja na vyama vya wachimbaji wa madini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amesema utekelezaji wa Sheria ya Madini na kanuni zake umeendelea kufungua fursa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini.

Alisisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha ukuaji wa Sekta ya Madini unaenda sambamba na kuimarika kwa biashara za ndani na kuongeza ajira kwa Watanzania.

“Serikali inatarajia kuona asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi zikizalishwa na kutolewa na Watanzania. Hili linahitaji usimamizi madhubuti wa sheria, pamoja na Watanzania kujiandaa kutumia fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini,” amesema Mavunde.

Aidha, aliwataka watoa huduma migodini kuunganisha nguvu, kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa ndani na kuboresha ubora wa bidhaa pamoja na huduma wanazotoa ili zikidhi viwango vinavyotakiwa na kampuni za uchimbaji wa madini.

Waziri huyo wa Madini alisema matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya yataongeza mahitaji ya bidhaa na huduma mbalimbali, hivyo ni wakati wa Watanzania kujiandaa kushindana katika soko.

Mavunde  pia alitoa angalizo kwa wawekezaji wote katika Sekta ya Madini kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za nchi. Alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, lakini wawekezaji wana wajibu wa kufuata taratibu zilizowekwa ili uwekezaji wao uwe na manufaa kwa Taifa na wananchi.

Akizungumzia mafanikio ya maboresho ya Sheria ya Madini, Mavunde alisema Serikali imeongeza ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini.

Alibainisha kuwa thamani ya ununuzi wa bidhaa na huduma katika Sekta ya Madini imefikia Shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, jambo linaloonesha ukubwa wa fursa zilizopo kwa wazalishaji na watoa huduma wa ndani.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Sekta ya Madini imezalisha ajira rasmi 20,421, ambapo ajira 16,695 zinashikiliwa na Watanzania.

Pia alisema nafasi za juu za uongozi katika migodi zimeendelea kushikwa na Watanzania, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo nafasi hizo zilikuwa zikishikiliwa zaidi na wataalamu kutoka nje ya nchi

Mavunde alisema mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa masoko ya madini 44 na vituo vya ununuzi wa madini 117 nchini, hatua iliyochangia kuongeza mapato ya Serikali kutoka Shilingi bilioni 161 mwaka wa fedha 2015/2016 hadi Shilingi trilioni 1.393 mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, alisema utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha hifadhi ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania umeiwezesha nchi kuwa na tani 28 za dhahabu na kuifanya miongoni mwa mataifa matano yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika, aliongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umefikia asilimia 10.1.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aliwataka watoa huduma migodini kuzingatia weledi, uadilifu na ubora wa huduma wanazotoa, huku akisisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Watanzania.

    

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG