Askofu Mkuu Kanisa Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa akifafanua jambo wakati alipokuwa akifungua Kongamanoa la kwanza la Wahudumu Wanawake wa kanisa hilo, lililofanyika Mkoani Tabora (PICHA ZOTE NA JOHN ISRAEL WA BANDA MEDIA)
Na John Israel, BANDA MEDIA- Tabora
JUMA lililopita mkoani Tabora kumefanyika kongamano kubwa lililowahusisha wahudumu wanawake wa kanisa Anglikana jimbo la Tanzania ambapo Dalili za wazi zimeonyesha jinsi Uongozi wa kanisa hilo hapa nchini ulivyoamua kuwasapoti wanawake katika huduma za kiroho, kijamii na kimaendeo.
Kongamano hilo lililowakutanisha wachungaji, Mashemasi na watawa lilianza, Agosti 12 -16,2026 katika kanisa kuu la mtakatifu Stefano, huku viongozi wakuu wa kanisa, Anglikana Tanzania wakihakikisha wahudumu hao wanawake wanapata kilichokusudiwa.
Askofu Mkuu kanisa Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mdolwa ndiye aliyefungua Kongamano hilo, siku wa Kwanza katika ibada maalumu ya ufunguzi iliyofanyika kanisani hapo, kisha kongamano likafanyika katika Ukumbi wa Canon. Nashon Nkugwe uliopo kanisani hapo
"Kanisa linatambua huduma ya Mwanamke hivyo kafanyeni kazi kwa kuzingatia wito, mlioitiwa katika Huduma Takatifu bila kusahau wajibu wa Ndoa kwa mlio na familia,
Nafurahi kuona huduma ya Wanawake inazidi kukua katika Kanisa, najua zipo baadhi ya Dayosisi ambazo bado hazijaanza kuamuru Wanawake, katika Huduma Takatifu si kwamba hazitambui huduma hiyo, ni jambo la Utaratibu” amesema Askofu Mkuu Dkt. Maimbo.
Ama kwa upande wake Makamu Askofu mkuu wa kanisa hilo Dkt. Dickison Chilongani ambaye pia ni Askofu wa DCT. Amesema wanawake wahudumu, wana ziada ya Uvumilivu na uaminifu kuliko hata baadhi ya Wachungaji wanaume, hivyo kuwataka kujiamini katika huduma.
"acheni kujidharau, wewe umesoma, una mwili wa nyama, umeokoka, ni kasisi, una pareshi kama ilivyo kwa wanaume lakini unajidharau kumbuka unapojidharau Wachungaji wanaume wana take Advantage," amesema
Amewataja wanawake kuwa ni wavumilivu na waaminifu hasa kwenye mambo ya huduma na fedha, "hivyo mkazo wangu ni kuwa tuendelee kuwatumia wanawake katika mazingira yetu", amesema Askofu huyo ambaye pia ni mkuu wa chao kikuu cha Saint John's cha jijini Dodoma kinachomilikiwa na kanisa hilo.
Aidha Dean huyo anasema DCT, inatambua na kuthamini Mchango wa wanawake katika kanisa, hivyo katika Dayosisi hiyo anayoiongoza ina zaidi ya Wahudumu 300, na kwamba kati ya hao wahudumu Wanawake ni 79 ambao hawajawahi kumuangusha kutokana na Uvumilivu na Uaminifu walionao kazini.
kwa upande wake Mhazini wa Jimbo, KAT ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Tabora, Elius Chakupewa anasema kwa sasa Nchini Tanzania ni Dayosisi 14 kati ya 28 zinazoweka mikono wanawake kuwa makasisi ambayo ni hatua kubwa na kwamba anaamini baada ya muda watafikia ngazi ya Uaskofu.
"1867 huko kwa wenzetu iliamliwa wanawake wawekewe mikono ya ushemasi na waishie hapo, lakini sasa wamepanda kufikia ngazi ya Askofu, hapa nchini kwetu bado kufikia ngazi hiyo lakini muda utaongea endeleeni kuchapa kazi", amesema
Nae Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Dkt. George Otieno Lawi anasema njia ya Mungu haipingiki, anasema yeye ni Mmoja kati ya walioaminishwaga kuwa ukuhani ni kwa wanaume, hivyo aliwahi kuwapinga waziwazi kuanzia kusoma, kuwekewa mikono na hata kutumika tangu wakati akiwa chuoni huko St. Philps Kongwa mkoani Dodoma.
Otieno anasimilia baadhi ya visa alivyokuwa akifanya pamoja na baadhi ya wanaume wengine aliosoma nao kuwa, "ilikuwa ikifika kipindi mwanamke anashirikisha Meza ya Bwana, mimi nikishika kikombe cha ushirika si mrudishii mpaka kwanza tuzungeke wanaume wote ndipo tunamrudishia", anasema Dkt. Otieno
Aidha anasema kilichomshtua baadae kuwa jambo la Mungu huwa halipingiki ni baada ya kumaliza masomo yake huko chuoni, St. Philps, ambapo vyuo alivyosoma baada ya hapo na hata vituo vya kazi alivyopangiwa alikuta viongozi ni wanawake.
"nawaambia jambo ambalo limekusudiwa na Mungu huwa halizuiliki, ili kulijua hilo baada ya Kongwa kila nilipoenda kwa kazi au kusoma nje na ndani ya nchi nilikuta viongozi ni wanawake, ikiwemo Msalato, ambako nilimkuta Kasisi Hilda kabia niliyewahi kumsumbua huko St. Philps ikabidi nitubu nakuanza kuwaunga mkono katika huduma", anasema na kuongeza
"unajua Mungu anapokwambia uende kilindini hakwambii uende ufanye unayoyataka, anataka ukafanye anayataka yeye mwenyewe, ndiyo maana tunapokiuka na kufanya tunayoyataka sisi tunajikuta katika majibizano makali,
katika juma hili la kongamano tumejifunza kuona upana katika utumishi, ikiwemo wahudumu kugusa maisha ya watu, hasa wenye uhitaji (injili ya matumaini) tuzame kilindini tukafanye ambayo hatukuyafanya kabla", amesema Otieno
Mkuu wa Chuo cha Theologia Msalato jijini Dodoma, Kasisi Can, Hilda Kabia na Mama Askofu Lilian Gaula wa Dayosisi ya Kondoa ni miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kuwekewa mikono ya Ukasisi Nchini Tanzania.Hao ndiyo waliokumbana na joto la kukatishwa Tamaa na kundi la akina Dkt. Otieno Huko Chuoni Saint Philps Kongwa wakati wakisoma.
Hayati Askofu Godfrey Mhogolo, enzi za uhai wake
wanasema pamoja na hali za kuzarauliwa, kukatishwa tamaa kijinsia kutokana na mfumo Dume ndani ya kanisa, wakati huo lakini wanawataja hayati Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo na Mkuu wa Chuo hicho wakati huo Canon Sange Wangoya, kuwa ndiyo waliowatia moyo wa kusonga mbele bila kukata tamaa.
"tunamshukuru Mungu sana leo kushuhudia kundi hili la wachungaji, makasisi wanawake na watawa zaidi ya 200 ndani ya kanisa la AnglikanaTanzania kwa kuwatumia, Askofu wa DCT Godfrey Mhogolo na mkuu wa Chuo cha St. Philps wakati huo, Canon Sange Wangoya hawakutuacha tuanguke", wanasema kwa nyakati tofauti.Canon William Sange Wangoya mkuu wa chuo cha Saint Phips 1994-1995
Akiongea kwa simu kutoka mkoani Mara, Canon Wangoya ambaye ni mkuu wa Chuo hicho wa 20, anasema kwanza anawashukuru wanafunzi wake hao kwa kumkumbuka, huku akikiri kuwa anajivunia ongezeko la wahudumu wanawake ndani ya kanisa, japo wakati alipokuwa akifundisha St. Philps aliamini kuwa wachungaji (Mapadri) ni wahudumu wa Meza ya Bwana na si warithi wa Ukuhani kama ilivyo kwa Wa Hi Church Wanaoamini kuwa Ukuhani ni wa wanaume huku wakiwa wamesahau kuwa Yesu alipokuja alimaliza hilo akitoa uhuru wa kila mtu kumtumikia.
Anasema alilazimika kutoa elimu ya usawa wa kijinsia katika huduma ya kanisa baada ya kugundua baadhi ya wanafunzi wa kiume wanafanya ubaguzi wa wazi dhidi ya wanafunzi wanawake kiasi cha kukataa hata huduma ya Meza ya Bwana.
Limbuko (chanzo) cha kongamano la Wachungaji wanawake ni mkoani Tabora nchini, Tanzania ambako wawakirishi wa makanisa mengine walialikwa kushiriki wakiwemo wachungaji wanawake kutoka Nyahururu huko nchini Kenya.
MWISHO





