Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam kujibu madai ya TEWUTA.
Baadhi ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mazungumzo ya Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi (hayupo pichani) alipozungumza na vyombo hivyo leo jioni.
Baadhi ya wanahabari wakifuatilia mazungumzo hayo.
Baadhi ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mazungumzo ya Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi (hayupo pichani) alipozungumza na vyombo hivyo leo jioni.
KAMPUNI ya
Simu Tanzania (TTCL) imepinga madai yaliyotolewa na Chama cha
Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania
(TEWUTA) jana dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na
kufafanua kuwa madai hayo si ya kweli zaidi ya upotoshaji wenye nia ovu
ya kufanikisha malengo binafsi na kutaka kuikwamisha jitihada za TTCL
katika maendeleo.
Meneja
Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo
Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam alisema madai
yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya
Wakurugenzi ya TTCL hayana ukweli wowote bali wahusika walilenga
kuupotosha umma.
"Menejimenti
ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma kuwa,
madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya
Wakurugenzi ya TTCL si sahihi. Hoja hizo zimejikita katika upotoshaji
wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi ya wahusika na kukwamisha
jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL
wenye nia na malengo ya kutekeleza mpango mkakakti wa kuiboresha na
kuiimarisha Kampuni ya Simu Tanzania.
Akifafanua
zaidi Meneja Uhusiano huyo wa TTCL alisema mwaka 2007 Kampuni ya Simu
Tanzania ilifanya mabadiliko ya Muundo wa Kampuni ili kuendana na hali
ya soko la Ushindani katika sekta ya mawasiliano na Muundo uliopo sasa
ni ule uliopitishwa na kuanza Kutumika mwaka 2007 baada ya kuidhinishwa
na kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema
menejimenti mpya ya TTCL iliyoanza kazi Februari 2013 iliainisha
changamoto mbalimbali za kibiashara na kutengeneza Mpango Mkakati
utakaoletab mabadiliko ya kibiashara na kuongeza tija, huku ikizingatia
mabadiliko ya Kibiashara na ushindani wa soko katika sekta ya
mawasiliano, Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya
Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri mwelekezi kwa njia ya Zabuni ili
kupitia na Kushauri juu ya Muundo Mpya wa Kampuni utakaoendana na
Mahitaji ya Kibiashara na kuleta ufanisi.
Aliongeza
kuwa matokeo ya Kazi ya Mshauri mwelekezi yamelenga kubadilisha muundo
wa Kampuni, Muundo wa Mishahara na Muundo wa utumishi. Mpango huu wa
Mabadiliko ya Kibiashara unategemewa kukamilika katika kipindi cha mwaka
2016. Aidha alifafanua kuwa muundo wa mishahara unaotumika hivi sasa ni
ule uliopitishwa Mwaka 2007 baada ya Kubadilika kwa Muundo wa Kampuni
kama ulivyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL.
"...Mfumo
huu uliiweka TTCL katika nafasi ya kukabiliana na soko la ajira
kimaslahi. Mfumo huu wa Mishahara ulizingatia pia matakwa ya kisheria
ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6/2004
zimeainishwa aina tatu za Mikataba ya Ajira. Yaani: Mkataba wa Ajira
usiokuwa na Muda Maalumu (Unspecified period of time), Mkataba wa Ajira
wa Muda Maalum (Fixed Employment contracts) na pia Mkataba wa Ajira wa
kazi Maalum (Special Task)..."
"...Hivyo
Muundo wa Mishahara uliopitishwa mwaka 2007 uliainisha madaraja ya
malipo na viwango husika ikiainisha aina ya mkabata, Mkataba wa Ajira
usiokuwa na Muda Maalum na Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum. Katika
muundo huu madaraja na ngazi za Mishahara zimegawanyika katika ngazi
Kumi (10) kuanzia TTCL 1 (Ikiwa ndio Kiwango cha Juu) hadi TTCL 10
(Ikiwa ndio kiwango kidogo) Muundo huu uko wazi na ndio unaotumika
kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania. Hakuna
ulipaji wa mishahara (Payroll) yoyote ya Siri inayotumika tofauti na
hiyo iliyoainishwa," alifafanua Meneja Uhusiano huyo katika taarifa
yake.
Akizungumzia
Kampuni ya Rubiem ambaye ni Mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa kufuata
taratibu sahihi za manunuzi ya Umma, alisema mchango wa kampuni hiyo
katika mpango wa mageuzi kibiashara ni mkubwa na unaonekana dhahiri
tofauti na madai yaliyotolewa.
"...Matokeo
ya kazi yake yataanza kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo huduma na
bidhaa mpya zitaingia sokoni. Mshauri huyu anatarajia kukamilisha kazi
yake katika robo ya kwanza ya mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba, hatua ya
Menejimenti kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote za
nyongeza nje ya mkataba wake wa kazi na TTCL.
Menejimenti
ya Kampuniya Simu Tanzania TTCL inaomba kutumia fursa hii kuwajulisha
Umma kwamba, hali ya Kampuni yao ni thabiti, utendaji wa kazi unaendelea
vizuri na jitihada mbali mbali za kuboresha huduma zinaendelea kwa
ufanisi mkubwa," alifafanua Bwana Mushi kwa wanahabari.
"...Menejimenti
ya Kampuniya Simu Tanzania TTCL inapenda kuujulisha Umma kuwa, oja zote
zilizotolewa na TEWUTA si za kweli, ni taarifa zilizopotoshwa kwa
makusudi, zikilenga kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada
kubwa zinazofanywa na Wizara ya Sayansi na Mawasiliano, Bodi ya
Wakurugenzi wa Kampuni, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye lengo
la kuifanya Kampuni kutimiza kikamilifu Wajibu wake kwa Umma. Ieleweke
pia kwamba, Muundo wa mishahara ya Watumishi wa Kampuni ya simuTanzania
TTCL uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa
Kampuni ya Simu Tanzania. Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi wote
wa TTCL iko idara ya Fedha na kusimamiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya
Simu. Hakuna Payroll yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo
iliyoainishwa, hakuna posho zozote zinalipwa kinyume na utaratibu."
alieleza Meneja huyo wa TTCL.
Tags
BIASHARA



