Mraghbishi
Noorkiyengop Mbaima toka kijiji cha Enguserosambu akisimama mbele ya
mifugo iliyokutwa msituni katika eneo lililoruhusiwa la msitu wa jamii
wa Enguserosambu
Ilikuwa
ni siku ya shangwe na furaha kwa wananchi wa kata ya Enguserosambu
wilayani Ngorongoro. Hii ni baada ya serikali kukubali ombi lao la
kusimamia rasilimali ya msitu wa Loliondo namba 2 unaopakana na vijiji
vinne vinavyokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wapatao 20,000
wanaotegemea mahitaji yao toka katika huo msitu.
Huu ni
msitu pekee ambao wananchi kwa kushirikiana na Mkuu wao wa wilaya, na
mashirika rafiki, wamefanikiwa kuishawishi serikali kuukabidhi msitu huo
kwao. Katika mchakato huo uliochukua miaka kadhaa wanawake toka katika
vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan wamekuwa mstari wa
mbele katika kufanikisha azma hiyo ya kubakiza msitu wao wa enzi
mikononi mwao. Akielezea furaha yake aliposikia msitu wa Loliondo namba 2
umekabidhiwa kwa wananchi, mraghbishi mwanamke Noorkiyengop Mbaima
alisema
“Mimi
mwenyewe nimefurahia, kwa sababu sisi akina mama tunategemea sana msitu
huu kwa mahitaji yetu. Huu msitu kama ungeondoka katika mikono ya jamii
basi tungeathirika sana sisi kina mama.” Umuhimu wa msitu huu kwa kina
mama ndio uliowapelekea wao kutunga na kuimba nyimbo za hamasa na
kutumbuiza, kushiriki kwa wingi katika vikao mbalimbali vya maamuzi
wakati wote wa mchakato huo.
Kwa
kuwa msitu huu ndio tegemeo lao katika kuendesha maisha ya kila siku.
Hakuna chochote ambacho kiliamriwa bila ya wao kuchangia na
kushirikishwa kuanzia utungaji wa sheria ndogongogo za usimamizi wa
msitu hadi kukabidhiwa rasmi msitu huo. “Nikichukulia mfano katika
mikutano yote ya vijiji. Kiukweli wanawake wamekuwa wanajitokeza kwa
wingi, kuliko makundi mengine yoyote. Hata ile siku ya uzinduzi wa msitu
walikuwa wengi zaidi,” anaelezea Jackson Nangiria
Ushiriki huu wa wanawake unatokana na ukweli kwamba wana uhusiano
wa karibu na msitu huo wa enzi wa Enguserosambu.Si kwa ajili yao tu
pamoja na watoto wao pia. Ni watoto hawa wa kike wenye majukumu ya
kujenga nyumba kwa kutumia miti inayotoka ndani ya msitu huu, ndio
wanaotembea na punda wakiwabebesha maguduria ya maji kwa umbali mrefu
wakitafuta maji ambayo chanzo chake kipo kwenye msitu huu. Wanapopata
watoto wanahitaji dawa za kuwaogeshea na dawa za uzazi ambazo zinatoka
kwenye msitu huu.
Wao
ndio wapishi katika familia zao hivyo wanahitaji kuni zinatokana na miti
iliyoanguka na kukauka ambayo inapatikana kwenye msitu huu. “Kina mama
wanafanya mitambiko ndani ya msitu huu wengine ambao hawakupata watoto
wanapatia hapo baada ya kuomba ndani ya msitu huu. Si hivyo tu ndani ya
msitu huu kuna dawa mbalimbali za asili kwa mfano mtoto akizaliwadawa ya
kumwogesha na kumnawisha hupatikana humo humo na nyingine ni za kunywa
kama maziwa na nyingine kwa ajili ya mama,” anaeleza mwanamama
mraghbishi Noorkiyengop Mbaima. Uwepo wa wanawake hawa wa Kimasai katika
kata ya Enguserosambu kiukweli unatokana na uwepo wa msitu huu. Huu
ndio msitu wa enzi ambao serikali ilipendekeza uwe chini ya usimamizi
wake kama ulivyokuwa msitnamba moja wa Loliondo.
Pendekezo hilo lilitolewa kupitia timu mbalimbali toka wizarani,
ofisi za kanda na halmshauri ya wilaya, ambazo zilitembelea kijijini
hapo kuomba kupatiwa muhtasari wa kikao cha kijiji kitakachopitisha ombi
hilo la serikali.
Ombi hilo linakuja kwa kijiji kwa sababu msitu huo umekuwa chini
ya usimamizi wa wananchi wa kata ya Enguserosambu kwa miaka mingi. Ni
wananchi hao ndio ambao wameutunza msitu huo pasipo Kuombwa wala
Kukabidhiwa na serikali. Na kwa kweli wameweza kuutunza kwa muda wote
huo. Miti haijakatwa, wananchi wamejiwekea sheria ndogondogo na pia
kuwakamata wale ambao wamekuwa wakiharibu msitu huo. Hivyo wananchi hawa
wamewajibika katika kuhakikisha msitu unabaki katika hali yake ya asili
pasipo kushurutishwa na mtu yeyote.
Kwa mantiki hiyo muhtsari uliokuwa unaombwa na serikali ya
halmashauri yan wilaya ulihiitaji baraka za wananchi, ambao hawakuwa
tayari kutoa sehemu ya uhai wao unaotegemea msitu huo. Hakuna
mwanakijiji aliyekuwa tayari kukubali ombi hilo. Na jibu lilikuwa ni
wazi kabisa kwamba ombi hilo lilitishia mustakabali wa jamii
zinazozunguka msitu huo ambazo ni vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua,
Orkiu na Naan. Hivyo wakati serikali ikipendekeza kuusimamia
msitu huo wananchi kwa upande mwingine wakaanza kuiomba serikali
iwaruhusu kuusimamia. Ni kama kichekesho pande zote zinaombana
kuusimamia msitu huo. Serikalikupitia halmashauri ya wilaya inasema
tunahitaji kuusimamia, na wananchi wanaiomba serikali hiyo hiyo
kuusimamia msitu huo. “Kwa kweli sisi kama wananchi wa Enguserosambu
tumeona kwamba huu msitu ukiondoka chini ya usimamizi wetu tutaathirika.
Kwa sababu msitu huu ni uhai wa wananchi wa hapa. Tukikosa huu msitu,
hatupati maji wala mvua, tutakosa chakula. Kwa kifupi tutakosa kitu
muhimu cha uhai wa jamii,” anaelezea mraghbishi Noorkiyengop
Mbaima.
Ndani ya msitu huu kuna miti ambayo wazee wanaitumia kwa ajili ya
shughuli za kimila pamoja na miti ya kiasili ambayo inatumika kwa
shughuli mbalimbali. Baadhi ya miti hiyo ni pamoja na Oroilieni ambao
unatumika kwenye shughuli za jadi, ujenzi na kiimani. Akifafanua kuhusu
mti huo Robert Kamakia anaelezea, “Huwezi kuingia jando bila kuwa na mti
Oroilieni. Kwa kuwa unatumika katika kufanya baadhi ya shughuli za
kimila. Mti mwingine ni Orikienyi ambao unatumika kama dawa ya kutibia
magonjwa ya aina mbalimbali kama homa, kifua, malaria na kadhalika. Mti
mwingine ni Ostiani ambao hutumika kwa ajili ya kivuli na kutunza maji.”
Hivyo
msitu huu una maana kubwa sana kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya
wazee, wanawake na vijana. K wa upande wa vijana kwa mfano, mila na
desturi za kimasai zinawataka kujitenga hasa pale wanapoingia ngazi ya
Morani. Ambapo hutakiwa kuweka kambi kwa ajili ya kuchinja ng’ombe na
kula nyama. Tukio hili huchukua mpaka mwezi mmoja wakati vijana hao,
wanapoazimisha sherehe hizo.
Tukio
hili linashirikisha matumizi ya miti mbalimbali kwa mujibu wa taratibu
zao. Supu wanazokunywa huchanganywa na baadhi ya majani ya miti hiyo. Ni
dhahiri ulaji wa nyama kwa mwezi mzima unahitaji pia matumizi ya dawa
za asili. Na ndio maana wamasai hawasumbuliwi sana na magonjwa
yanayotokana na ulaji mwingi wa nyamba. Si hivyo tu porini hamna vitanda
hivyo baadhi ya majani hutumika kwa ajili ya zoezi hilo.
“Kiukweli
bila msitu vijana hawawezi kufanya chochote. Kwa kuwa kila kitu
kinatoka katika huo msitu,” anafafanua Julius Long’oli. Lakini si hivyo
tu, wakati wanaingizwa jando pia kuna miti inayotumika. Vivyo hivyo na
katika sherehe za kumaliza jando. Hivyo msitu ni sehemu ya mila na
utamaduni wa jamii hizi zinaouzunguka. Ni imani yao pia, ambayo kimsingi
ni lazima iheshimiwe. Huu ni msitu wao wa enzi na enzi. “Huu ni msitu
wa jamii kwa Kimasai unaitwa Elieteti yaani ndani ya jamii kwa maana ya
jina hilo ni msitu unaosaidia jamii ya sasa na ya kizazi kijacho. Kwamba
huu msitu unategemewa na kizazi cha sasa na kijacho,” anafafanua Yohana
Tuluni mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya kusimamia msitu. Mtizamo huu
wa wananchi wa kata hii, kwamba wao ndio wausimamie msitu huu, unatokana
hali halisi ya msitu namba moja wa Loliondo unaosimamiwa na serikali
kupitia halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kuwa katika hali ya
kutoridhisha. Miti mingi imekatwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi na
hivyo kutishia uhai wa msitu huo. Kitu ambacho wana Enguserosambu
hawakupenda kitokee kwa msitu namba mbili wa Loliondo ambao wanautegemea
kwa mustakabali wa maisha yao. Msitu huu umekuwa ukitegemewa na jamii
ya hapa kwa miaka mingi. Ni wao ndio ambao wamekuwa wakiutunza na kwa
kweli wamefanikiwa kwa njia moja ama nyingine kuufanya uwe mzuri zaidi
kuliko hata ule wa Liliondo moja unasimamiwa na serikali.
“Wazo la kutaka kumiliki msitu lilikuwa kama ndoto, ukiangalia na
hali halisi ilivyokuwa. Ni maono ya mtu mmoja aliyewashirikisha wenzake.
Mwishowe wazo likatolewa Kwa wanakijiji ambao waliungamkono wazo hilo.
Na mwishowe tukamwandikia Mkuu wa Wilaya na kwa kweli alituunga mkono
sana,” anafafanua mraghbishi na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Jackso
Nangiria Mchakato wa kuomba hadi kukabidhiwa usimamizi wa msitu
umewezesha wananchi wa Enguserosambu kuongeza ufahamu wa mambo
mbalimbali juu ya usimamizi wa misitu lakini pia mahusiano baina ya
wananchi na viongozi yameboreka zaidi.
Umoja
ni nguvu utengano ni udhaifu, hivi ndivyo unavyoweza kusema
Wanaenguserosambu wamekuwa wamoja zaidi. Mashirika rafiki yamesaidia
sana katika kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wao ambao maarifa hayo
yamewezesha kujiwekea mikakati na hatimaye kufanikisha jamii kumiliki
msitu wake wa enzi kwenye mikono yake. Wakati mchakato unaanza palikuwa
na kijiji kimoja tu cha Enguserosambu kilichokuwa kinaundwa na vitongoji
vinne vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan ambavyo sasa vimepata
hadhi ya kuwa vijiji. Kwa sasa sauti yao ni kubwa zaidi kuliko pale
Mwanzo.
Watendaji wa PALISEP wakiwa pamoja na wanajamii wakishikana mikono
kuonesha ushirikiano baina yao. Kuanzia kushoto ni Sarah Saningo,
Robert Kamakia, Jackson Nangiria, Norkiyengop Mbaima, Sunde Tutayo na
Fredy Samberu
Hivyo Bodi ya Wadhamini ilichaguliwa na mkutano mkuu wa kijiji,
ambacho sasa kina hadhi ya kata. Kwa hiyo usimamizi wa msitu huu kwa
sasa umekabidhiwa kwa Kata ya Enguserosambu. Hivyo wananchi kutoka
katika kila kijiji walichagua wawakilishi wao waliounda Bodi ya
Wadhamini. Wawakilishi hawa jukumu lao kubwa ni kuratibu mchakato wote
wa uombaji usimamizi wa msitu wa Loliondo 2.
Baada
ya kuchaguliwa wajumbe walipatiwa mafunzo na shirika la PALISEP ambao
pia walisaidia uandikishwaji wa bodi tarehe 12/09/2012. Bodi hiyo
imeundwa na wajumbe 10 kati ya hao wanawake ni 4. Bodi hii ilipata
mafunzo ya sheria mbalimbali za misitu, usimamizi wa misitu na bodi
yenyewe pia kupitia video ya hali ya msitu wa Loliondo 1. Walipata pia
ziara za mafunzo kwa kutembelea misitu inayosimamiwa na jamii kwa mfano
msitu wa Suledo uliopo Manyara wilaya ya Kiteto. Bila jamii kujitoa kwa
hali na mali isingewezekana kufanikiwa kwenye hili. Kwani bodi ya
wadhamini imefanya kazi kubwa. Jamii imeshiriki katika kuandika katiba
ya bodi na sheria ndogondogo ambazo zimepitishwa katika mikutano ya
vijiji.
“Baada ya kuchaguliwa jukumu letu ilikuwa ni kutembelea msitu ili
kujua hali yake. Lakini pia tuliweza kutoa elimu kwa wale waliokuwa
wanaishi na kufanya shughuli za kilimo ndani ya msitu. Ili waweze
kuondoka. Si kazi rahisi,” mjumbe wa Kamati ya Bodi ya Wadhamini Sunde
Tutayo.
Kwa sasa mpango ni kuboresha na kutunza vyanzo vya maji. Kupitia
bodi hiyo, wananchi wamejiwekea malengo ya kuuongeza zaidi kwa kupanda
miti zaidi. Hili linafanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa kuna baadhi ya
miti si rafiki mzuri kwa vyanzo vya maji inayakausha. Lakini si hivyo
tu Bodi ya Wadhamini inaangalia njia sahii ya kuhakikisha kwamba
zinapatika fedha za kununulia miti mipya. Wazo lililopo ni kuwakilisha
mtizamo huu kwa wanajamii ili waweze kutaarifiwa na kusikilizwa nini
yatakuwa maamuzi yao kwenye uchangishaji huo wa fedha. Changamoto
nyingine ni uboreshwaji wa sheria ndogondogo kwa kuwa hakuna mipaka ya
majukumu baina ya Bodi ya Wadhamini na Halmashauri ya serikali za
vijiji. Kuna umuhimu wa suala hili kuwekewa utaratibu mzuri wa
kiuwajibikaji kwa sababu muda mwingine vyombo hivi vinaweza kugongana
kimawazo na kiutendaji na nani anawajibika kwa nani.
“Hapo nje kuna mikaratusi tumeikamata sisi kama Bodi ya Wadhamini.
Mtu ameangusha mti mbichi ambao haujakauka. Na ameiyangusha bila
idhini. Tumefanya hivi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Diwani.
Tunachosubili tukae na serikali ya kijiji ili tujue tunafanya nini,”
anafafanua mraghbishi na Kaimu Katibu wa Bodi ya Wadhamini Jackson
Nangiria. Kwenye kukabidhiwa msitu mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya
na Diwani wa Kata ya Enguserosambu walikuwepo wakati wa kukabidhiwa kwa
msitu huo pamoja na wenyeviti wa vijiji vyote vinavyounda kata ya
Enguserosambu. Kwa hakika wenzetu wa Enguserosambu wameweza kujipanga na
kuhakikisha kwamba msitu wao wa enzi unabaki mikononi mwao.
Tags
HABARI KITAIFA