Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ametembelea kiwanda cha kusindika tumbaku cha mkoani Ruvuma na
kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.
Akizungumza jana jioni(Jumanne,
Januari 5, 2016), katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea,
wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo,
Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa
pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Waziri Mkuu amesema, Serikali ina
dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo
la kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John
Pombe Magufuli la kufufua viwanda nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea
maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua
ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa
iliyopita baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji.
Pia, amemtaka Afisa Biashara
kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na
kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika
tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha
Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe
Mahakamani.
“Serikali imeazimia kufufua
viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe,
Tunahitaji kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia,
amesikiliza na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa tumbaku wa Mkoa
huo, ambao walilalamikia mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo
vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao hadi kushindwa kuendelea kulima
zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.
Aidha, Waziri Mkuu amewasihi
wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa
viongozi wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha
za wakulima kiashi cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011
hadi 2014 tayari wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia,
amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na
wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima
kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja
mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi.
Amewashauri wakulima kuunda na kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake
mkoani Ruvuma, atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana
na viongozi wa Chama na Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.
Tags
HABARI KITAIFA