BANDA MEDIA BLOG

BLACK SAILORS YAZIDI KUWEKA HISTORIA MPYA ZENJ


sailors
Na Abubakar Kisandu, Zanzibar
Timu ya Black Sailors yenye maskani yake Magomeni Jitini ambayo inashiriki ligi kuu soka Zanzibar Kanda ya Unguja kwa sasa ndio timu pekee ya Mitaani ambayo inafanya vizuri katika ligi kuu soka ya Zanzibar kanda ya Unguja wakiwa wana alama 25 kwasasa wakishika nafasi ya 3 kwenye msimamo.
Jana usiku walifanikiwa kuwafunga vinara wa ligi hiyo ambao pia ni wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika JKU, kwa bao 1-0 bao pekee lililofungwa na Abdul Azizi Seif (Ngasa) mchezo uliochezwa katika Dimba la Amaan.

Sailors ndio timu pekee kwa msimu huu iyozifunga timu 2 zinazoshiriki michuano ya kimataifa (Mafunzo na JKU) ambao ni bingwa mtetezi na makamu wanaowakilisha Zanzibar katika mashindano ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mbali ya rekodi hiyo pia Sailors ina rekodi nyingine nzuri ya kuwa ndiyo timu pekee mpaka sasa imecheza michezo mitatu mfululizo bila ya lango lake kuruhusu kufungwa hata bao moja.
Michezo hiyo mitatu mfululizo Sailors ilicheza jana ikafanikiwa kuifunga JKU bao 1-0, mchezo mwingine walicheza tarehe 16/02/2016 na timu ya Polisi na walimaliza kwa sare ya 0-0, na tarehe 02/02/2016 Sailors waliifunga bingwa mtetezi Mafunzo mabao 3-0.
Hivyo imecheza michezo mitatu mfululizo pasipo kufungwa hata bao moja na hii inaonesha kuwa ina ulinzi imara kwasasa hasa baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo.
Rekodi nyingine iliyowekwa na Sailors katika ligi kuu soka Zanzibar Kanda ya Unguja mpaka sasa haijawahi kufungwa na timu yoyote ya Mitaani kama vile Miembeni, Kimbunga, Mtende Rengers, Jangombe Boys, Kijichi na Chuoni.
Mbali na rekodi hiyo, Sailors haijafungwa na timu zote za vikosi vya Muungano yani timu ya Polisi na wana Jeshi Kipanga ambapo katika michezo miwili waliyokutana Sailors na Polisi , mmoja Sailors ilishinda na kwenda sare mchezo mmoja.
Black Sailors mpaka sasa imeshacheza michezo 15, ambapo imeshinda michezo 7, wameenda sare michezo 4 na kufungwa michezo 4, ambapo michezo yote hiyo waliyopoteza mzunguko wa mwanzo wamefungwa na baadhi ya timu za Vikosi vya S.M.Z wakiwemo KVZ, JKU, KMKM na Zimamoto.
Black Sailors ilianzishwa tangu mwaka 1981 ambapo huu ni msimu wake wa kwanza kucheza ligi kuu soka Zanzibar tangu kuanzishwa kwake na kwasasa inaonekana kuwa ni timu tishio kufuatia vipaji vingi alivyovisajili kocha mkuu wa timu hiyo  Juma Awadh.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG