Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Ni jambo lisilopingika kokote duniani kuwa afya bora ndio chanzo cha maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Afya ikiwa bora binadamu anakuwa na uwezo wa kuwaza na kufanya mambo mbalimbali yenye tija kwake na kwa taifa lake.
Kwa kuonyesha kujali afya zetu,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ilianzisha Mfuko wa Afya ya Jamii
ujulikanao kama CHF ambao ulianza kwa majaribio wilayani Igunga, Mkoa
wa Tabora mwaka 1996 na kuanza rasmi 2001 baada ya bunge kupitisha
muswada huo.
Chimbuko hasa la kuanzisha Mfuko
wa Afya ya Jamii ni kupungua kwa rasilimali na vyanzo vya mapato vya
kuhudumia sekta ya afya hivyo kusababisha kudorora kwa huduma hiyo
ambapo inasababisha wananchi kutopata matibabu yanayotakiwa na wengine
kuacha kabisa kwenda kupata huduma katika vituo vya afya kwa kuwa
gharama za matibabu ni kubwa.
Mfuko wa Afya ya Jamii yaani CHF
ni utaratibu wa hiari unaomuwezesha mtu binafsi,vikundi au kaya kupata
huduma za matibabu kwa mwaka mzima kwa kuchangia kiasi cha shilingi 5000
hadi 20000 kwa kadri ya uwezo wa mtu au jamii yenyewe kulingana na
Halmashauri husika itakavyoamua.
Kiasi hiki cha kuchangia kwa
mwaka kinaweza kupatikana hata kwa mtu mwenye kipato cha chini kwakua
kiwango hiki ni sawa na bei ya kuku mmoja, uchangiaji huu ndiyo
uliyomfanya aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Yahaya Nawanda kuja
na kauli mbiu isemayo “Kuku mmoja, matibabu mwaka mzima”. Uhamasishaji
huu ulisaidia sana watu wengi kujiunga na CHF katika wilaya hiyo.
Na kama iliwezekana katika
Halmashauri ya Iramba kwa kuku mmoja kugharamia matibabu ya kaya
kwa mwaka mzima, tunaamini kuwa kauli mbiu hiyo inaweza kufanya kazi pia
katika Halmashauri nyingine iwapo kila kiongozi aliyekabidhiwa dhamana
ya kusimamia maisha ya watu atadhamiria kuwapa wananchi huduma bora za
matibabu kwa utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua.
Tags
HABARI KITAIFA