……………………………………………………….
Na Magreth Kinabo-MAELEZO
Serikali imesema itaendelea
kudumisha na kuimarisha mahusiano ya kideplomasia kati ya nchi rafiki
na wadau wa maendeleo ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025 na kutimiza malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu
wa Milinea (MGDs) ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni hatua ya kuhakikisha
inapunguza kiwango cha umasikini na kuboresha maisha ya watu nchini.
Hayo yalisemwa leo na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya
kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 iliyoshirikisha mabalozi mbalimbali
wanazoziwakilisha nchi zao hapa nchini iliyofanyika leo jioni Ikulu
jijini Dar es Salaam.
“Hivi sasa Uchaguzi Mkuu wa
Tanzania Bara umekwisha. Ni wakati wa kufanya kazi na kauli mbiu yangu
ni “Hapa Kazi Tu”. Serikali mpya ya Awamu ya Tano imekuja na mkakati wa
kuboresha na kuimraisha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili
kusisitiza nidhamu na utendaji kazi, kuhesimu haki za binadamu, utawala
bora na kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania wanapata maendeleo
endelevu ya kiuchumi na kijamii,”alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga aliongeza kwamba
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameiacha nchi ikiwa imara na marafiki wengi,
pia uchumi wake umekuwa katika kiwango cha asilimia saba (7) kwa
kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Alisema mafanikio hayo yametokana
na juhudi za ushirikiano na misaada yao, hivyo aliwashukuru kwa michango
yao waliyoifanya hapa nchini.
“Ninawaomba muendelee kutusaidia
kwa kuwa hivi sasa tuna mipango ya maendeleo ambayo ina lenga kuboresha
maisha ya Watanzania wote hususan wale wanaoishi katika kiwango cha
chini cha umasikini,”alisema Balozi Mahiga.
Alizitaja changamoto kubwa
zilizopo katika kutimiza malengo hayo ni kuwepo kwa hali ya umasikini
nchini, ukosefu wa ajira na rushwa. Hivyo Serikali inafanya kila
jitihada za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa bila ya kufanya
hivyo itakuwa ni vigumu kutimiza malengo ya nchi ya kufikia uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Balozi Mahiga alisema kwamba ili
kutimiza malengo hayo, Serikali hivi sasa inaendelea kudhibiti matumizi
ya fedha za Serikali, kujenga nidhamu, uwazi na uwajibikaji katika
matumizi hayo ndani ya Serikali na hata kwa sekta binafsi na kuimarisha
maeneo ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Serikali imesema kwamba
itaendelea kuendeleza ushirikiano huo, ili kuweza kupambana na vitendo
vya rushwa, biashara haramu ya binadamu, ugaidi na matumizi ya silaha.
“Tunawaomba mtusaidie husasan
kwenye eneo la upatikanaji wa taarifa, kujenga uwezo na masuala ya
kiufundi katika kukabiliana na vitendo hivi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu suala la
Uchaguzi wa Zanzibar, Balozi Mahiga alisema Zanzibar inajitegemea katika
masuala ya kisiasa na kiutamaduni licha ya kuwa ni sehemu ya Muungano
wa Tanzania.
Balozi Mahiga alifafanua kuwa
Zanzibar ina Katiba yake, Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi .Hivyo
kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 ulifutwa kwa
sababu mbalimbali kama ilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar(ZEC).
Aliongeza kwamba mazungumzo ya
kufikia muafaka wa suala hilo, yanaendelea ma uchaguzi mwingine
utafanyika Machi 20, mwaka huu. Hivyo mazungumzo hayo bado yanaendelea
ili kuufanya uchaguzi huo uwe huru, haki na uwazi ili kukidhi viwango
vya kimataifa vya demokrasia.
Tags
HABARI KITAIFA