Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Taasisi binafasi ya Karibu Tanzania
Association (KTA) kwa pamoja wamezindua programu ya maendeleo ya soka
kwa wanawake vijana ili kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji
kijamii na kiuchumi kwa wanawake nchini itakayofadhiliwa na Shirika la
Forum Syd kutoka nchini Sweden.
Uwekaji saini wa mkataba huo wa
ushirikiano umefanywa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mia
Mjengwa Bergdahl, Mratibu wa Programu hiyo kutoka taasisi ya Karibu
Tanzania Sweden katika ofisi za TFF zilizopo Karume.
Programu hiyo ni ya aina yake
ambayo haijapata kufanyika nchini inalenga kujenga mfumo utakaotumiwa
nchi nzima katika kutoa elimu na mafunzo kwa soka la wanawake kwenye
maeneo ya ufundi (makocha), waamuzi (refarii), uongozi na tiba kwenye
michezo.
Pia itawezesha kuendeleza vipaji
kwa wachezaji wanawake vijana na kuongeza hali ya kujitambua na
kujiamini kwa walengwa. Lengo ni kuongeza idadi ya wachezaji wenye ubora
na viwango kwa soka la wanawake vijana katika ngazi zote, hivyo
kuifanya programu hii kuwa nyenzo katika kuwawezesha wanawake.
Kwa kuanzia kozi 20 za soka la
wanawake vijana kwenye Vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi zitaanzishwa
kwenye kanda saba. Jumla ya wanawake vijana 600 ikiwamo 30 kutoka
katika kila chuo cha Maendeleo ya Wananchi watashiriki.
Katika programu hii, Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanashiriki kikamilifu
kwa kuwezesha wanafunzi na miundo mbinu ya vyuo vya maendeleo ya
wananchi vilivyo chini ya wizara hiyo kutumika katika kufanikisha
programu hii.
Mafunzo yatatolewa sambamba na
mafunzo mengine ya kawaida yanayotolewa kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya
Wananchi, kama vile maarifa ya jumla na mafunzo ya ufundi.
Tags
MICHEZO KITAIFA