Na. Lilian Lundo – Maelezo
Timu ya mchezo wa Tenisi kwa
walemavu (wheelchair tennis) ya Tanzania imeshika namba mbili Afrika
katika mashindao ya mchezo huo yaliyofanyika hivi karibuni jijini
Nairobi.
Hayo yalisemwa na kocha wa timu
hiyo Bw. Riziki Salum leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na
vyombo vya habari juu ya ushindi walioupata.
“Tumeshiriki zaidi ya mashindano
mawili jijini Nairobi na tumekuwa washindi wa pili Afrika, timu zote
mbili za wanawake na wanaume zimeingia fainali zikiwa na na jumla ya
wachezaji saba wakiongozwa na nahodha Juma Mohamedy,” alisema Salum.
Salum aliongeza kwa kusema, chama
cha Dunia cha mchezo huo kimeahidi kuwapa mualiko wa kushiriki
mashindano ya Dunia yatakoyofanyika Japan mwaka huu kulingana na ratiba
itakayopangwa.
Aidha, Bw.Salum alimshukuru
mfadhili Bi. Latya Nassoro ambaye ameiwezesha timu hiyo kwenda kushiriki
mashindano hayo kwa kuwalipia nauli ya kwenda na kurudi pamoja na
malazi na chakula.
Kwa upande wake Bi. Latya Nassoro
aliwahimiza na kuwaomba watu binafsi na makampuni kujitokeza kufadhili
timu za Tenisi ili mchezo huo ufike mbali nchini na kupata ushindi ambao
utarejesha makombe nyumbani na kuiletea nchi sifa na kuitangaza
miongoni mwa mataifa kupitia mchezo huo.
Timu hiyo ya Tenisi ilishiriki
mashindano ya Dunia yaliyofanyika mwaka 2013 nchini Uturuki na kushinda
kombe la timu bora zilizoshiriki katika mashindano hayo.
Tags
MICHEZO KITAIFA