Mwenyekiti
wa SHIWATA, Cassim Taalib (aliyesimama) akizungumza na wanachama
(hawapo pichani) maandalizi ya sherehe za kumkabidhi eneo mchezaji bora
wa Afrika , Mbwana Samatta katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam juzi
Mwigizaji maarufu nchini, Ahmed Olotu maarufu kama mzee Chilo akizungumza na wanachama wenzake wa SHIWATA katika mkutano huo
……………………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umesogeza mbele kwa
siku moja sherehe za kumkabidhi eneo mchezaji bora wa Afrika, Mbwana
Samatta hadi Juni 5, 2016 ili kupisha pambano kati ya Timu ya Taifa ya
Tanzania (Taifa Stars) na timu ya Taifa ya Misri.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassima Taalib alisema jana Dar es
Salaam kuwa maandalizi ya sherehe hizo ambazo awali zilipangwa
kufanyika Juni 4, 2016 yamekamilika na Mbwana atakabidhiwa hekari tano
za eneo ambazo atalitumia kujenga Kituo cha wanamichezo katika eneo la
Mwanzega, Mkuranga mkoa wa Pwani.
Alisema hivi karibuni baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee Ali
Samatta alishukuru SHIWATA kutambua mchango wa mwanae katika medani ya
soka nchini na kuahidi kusaidia kusimamia juhudi za mwanae katika
kuendeleza michezo nchini.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Salum Madadi alithibitisha kufanyika mchezo wa Stars na Misri siku
ambayo awali ilipangwa Mbwana kukabidhiwa eneo hilo.
Samatta anayecheza soka ya kulipwa Ulaya atatumia mapumziko
ya mechi ya Stars na Misri kukabidhiwa eneo hilo na kadi ya uanachama wa
SHIWATA katika kutambua mchango wake kuitangaza Tanzania kuwa mchezaji
bora Afrika kati ya wachezaji wanaocheza mpira wa kulipwa ndani ya bara
la Afrika.
Katika sherehe hizo wasanii 35 watakabidhiwa nyumba zao kati
hiyo, wanachama watatu watakabidhiwa nyumba ndogo, 31 watakabidhiwa
misingi na nyumba kubwa moja na kufikia idadi ya nyumba 185 ambazo
zimekwisha jengwa kijijini hapo mpaka sasa.
Akizungumza katika mkutano wa
wanachama kujiandaa na sherehe hizo walimuomba Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Mnauye awe mgeni rasmi ambapo pia
waliomba dua la kumuombea Rais John Pombe Magufuli katika juhudi zake za
kupambana na wabadhirifu wa mali ya umma.