BANDA MEDIA BLOG

TAARIFA YA MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU

logoSerikali kupitia Wizara yangu inaendelea na utaratibu wa kutoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini kila wiki kama tulivyoahidi. Takwimu za ugonjwa huu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 22 Mei 2016, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 21,585  ambao wametolewa taarifa ya kuwa na ugonjwa huu, na kati ya hao, ndugu zetu 338 wamepoteza maisha.
Tumefarijika kuona takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2016 zinazoonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua kwa asilimia 49 (karibu nusu ya wagonjwa), ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 108, na hakuna aliyepoteza maisha, ikilinganishwa na wagonjwa wapya 212 walioripotiwa wiki iliyotangulia ya Mei 9 hadi 15.

Mikoa ambayo imeripoti wagonjwa wiki hii ni Morogoro (47), Manyara(16), Lindi (14), Mara (11) Dar es Salaam (9), Pwani (6), Kagera (2), Kilimanjaro (2) na Iringa (1).
Halmashauri zilizoongoza kutoa wagonjwa wengi ni Kilosa (27),  Mvomero (15), Kilwa (14), Tarime Mjini (11), Babati Vijijini (10), Kinondoni (9), Babati Mjini (5), Morogoro Mjini (5), Kibaha Mjini (4), Bukoba Mjini (2), Chalinze (2), Same (2), Iringa Mjini (1) na Mbulu (1).
Katika wiki iliyopita, mikoa ambayo haikuwa na wagonjwa wa kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Mwanza, Geita, Singida, Shinyanga, Arusha, Tanga, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu na Mtwara. Na mikoa ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa wa kipindupindu tangu mlipuko uanze ni Ruvuma na Njombe
Kupungua kwa idadi ya wagonjwa kusirudishe nyuma juhudi za kuuzuia ugonjwa huu, bali tunatakiwa kuzidisha jitihada ili tuweze kuuondoa, tusiwe na wagonjwa kabisa. Ni vema kuchukua tahadhari zaidi, hasa katika msimu wa masika, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa maji ya mvua kusambaza vimelea vya ugonjwa huu. Tuendelee kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG