BANDA MEDIA BLOG

HANS KATIKA SAJILI 3 ZA KISHABIKI, DANTE WA NINI YANGA SC?


Dante 2
Na Baraka Mbolembole
Mlinzi wa kulia Hassan Kessy, kiungo wa mashambulizi Juma Mahadhi na sasa mlinzi wa kati Vicent Andrew wamesaini kujiunga na mabingwa mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania bara, timu ya Yanga SC.
Kessy amesajiliwa kama mbadala wa Juma Abdul na Mbuyu Twite ambao wamefanya vizuri katika nafasi hiyo ya beki namba mbili kwa misimu minne sasa. Kessy ni mchezaji mzuri katika kupandisha mashambulizi, mtengenezaji wa nafasi za magoli. Naweza kusema usajili wake wa kutoka Simba SC hadi Yanga ‘ni kamari’ itakayoamuliwa na jitihada zake mwenyewe.

Kwa tuliomuona Kessy tangu akichipukia Mtibwa miaka mitatu iliyopita hatuna shaka kuhusu uwezo wake ndani ya uwanja. Usajili wa Mahadhi kutoka Coastal Union siwezi kuzungumzia kwa maana sijaona kitu kipya kutoka kwa kiungo huyo ambacho atakiongeza katika nafasi hiyo ambayo tayari kuna wachezaji mahiri zaidi yake kama Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke.
Said Juma Makapu na Salum Telela nadhani wanastagli kubaki katika timu hiyo kwa kupewa mikataba mizuri yenye maslahi bora kwa maana wamekuwa na mchango mkubwa sana ndani ya uwanja.
Sababu za majeraha ya mara kwa mara kwa Telela na Makapu yanaweza kumstua mkufunzi Hans Van der Pluijm na kumfanya kusaini kiungo wa ziada, lakini alipaswa kuwa mwenye uwezo zaidi ya Mahadhi ambaye si tu atatimiza majukumu yake vizuri kwa kuichezesha safu ya mashambulizi, bali mwenye kufunga magoli muhimu yasiyotarajiwa katika nyakati ngumu.
Dirisha la usajili bado liko wazi. Yanga wanacheza nane bora ya makundi ya Shirikisho Afrika, pia wana nafasi ya kuiwakilisha Tanzania bara katika CECAFA Kagame Cup, pia watakuwa na michuano ya FA Cup na ligi kuu msimu ujao. Ni michuano mingi kwa kweli hivyo wanapaswa kuwa na kikosi bora kipana.
VICENT ANDREW ‘DANTE’ SI USAJILI MWAFAKA Kwa kipindi hiki safu ya beki ya kati ya Yanga ina walinzi watano, wale wa kigeni ni Mbuyu Twite na Mtogo, Vicent Bossou, pia kuna walinzi wazawa watatu, Kelvin Yondan, Pato Ngonyani na nahodha, Nadir Haroub.
Sikatai ubora wa Andrew, ndiyo maana hata katika kikosi bora cha msimu uliopita nilimpanga sambamba na Bossou katika beki ya kati lakini ukitazama sajili hii, ni wazi Yanga wamemsaini beki huyo aliyekuwa Mtibwa Sugar kwa sababu pia alikuwa katika ‘rada’ za usajili katika klabu za Simba na Azam FC.
Andrew amekubali kwenda Yanga labda kwa sababu za kimaslahi, kama ni kimpira atakuwa amejiweka njia panda kwa maana anaondoka Mtibwa baada ya misimu miwili ya kujipambanua kama mlinzi bora wa kati na kwenda sehemu ambayo tayari baadhi ya walinzi wa nafasi hiyo wamekuwa wakihamishiwa katika nafasi ya kiungo namba 6 kufuatia wingi wao.
Inawezekana akapata nafasi ya kucheza kwa maana katika siku za karibuni walinzi Kelvin na Nadir wamekuwa wakipata majeraha ya mara kwa mara. Kusubiri nafasi ya majeruhi ili kucheza Yanga na kwenda Azam au Simba ama kubaki Mtibwa ilikuwa ni uamuzi sahihi zaidi kwa Andrew.
Nimekuwa nikiamini sana sajili za Hans lakini si kwamba zote zimekuwa na matokeo bora. Malimi Busungu, Paul Nonga, Mniger, Boubacar, Mghana Joseph Zuta, kipa Benedict Tinoco ni baadhi ya sajili za Mholland huyo ambazo hazijalipa.
Usajili wa Andrew kutoka Mtibwa kwenda Yanga na ule wa Mahadhi kutoka Coastal na kujiunga Yanga unafuata ‘mkumbo’ wa sajili ya Malimi Busungu msimu uliopita alipotoka JKT Mgambo na kujiunga Yanga. Hizi ni sajili tatu za kishabiki zaidi ambazo Hans amezifanya klabuni Yanga.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG