Waamuzi wanne kutoka Ethiopia,
ndio watakaochezesha mchezo wa kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Vijana
wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na Shelisheli
utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kuwania nafasi
ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa kwa vijana wenye umri wa chini ya
miaka 17. Waamuzi hao ni Belay Tadesse Asserese ambaye ni mwamuzi wa
kati wakati wasaidizi wake ni Tigle Gizaw Belachew upande wa kulia na
Kinfe Yilma Kinfe upande wa kushoto huku mwamuzi wa akiba atakuwa Lemma
Nigussie. Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Bester Kalombo.
Serengeti Boys ilikuwa kambini
tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mchezo huo wa kufuzu fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa Shelisheli utakaofanyika
Juni 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Mchezo
wa marudiano kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2,
2016 huko Shelisheli.
Katika kuajindaa na mchezo huo,
Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya
vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth
Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu
katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kadhalika Serengeti Boys ilicheza
mfululizo michezo saba ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2),
India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo
ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20
bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Katika mashindano ya AIFF, timu
hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki katika
jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika hatua za juu katika
mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani
CONCACAF (USA) na AFC (India, Korea na Malaysia).
Awali timu ya Serengeti Boys
ilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kwa sababu ya rekodi zilizokuwa
zinaiweka Tanzania katika viwango vya chini katika umri huo kwa nchi za
Afrika Magharibi na Kaskazini zilikuwa juu zaidi na vilevile ukweli wa
kwamba timu kama USA, Korea, Malasyia na India zilikuwa na bajeti kubwa
iliyogharamiwa na Serikali zao na walikuwa na vifaa vya kila namna kiasi
cha kuomba magari kwa ajili ya vifaa vya mazoezi na mechi.
Serengeti Boys ilimaliza
Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao
3-0. Serengeti Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na
awali walipokutana walitoka sare ya 2-2
MWAMUZI WA ANGOLA KUWAAMUA YOUNG AFRICANS, TP MAZEMBE
Mchezo wa kuwania Kombe la
Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans ya Dar es Salaam,
Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
utachezeshwa na Mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia
Sikazwe atasaidiwa na Jarson
Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line
1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2)
huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba. Kamishna wa
mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa Rwanda. Pia mchezo huo
utakuwa na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.
SUALA LA STAND UNITED YA SHINYANGA
Kutokana na mkanganyiko wa
uendeshaji wa mchakato wa uchaguzi katika Klabu ya Stand United ya
Shinyanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF), limeagiza
michakato yote miwili inayoendeshwa sambamba ndani ya klabu ya Stand
United, isimamishwe mara moja kisha kusubiri maelekezo mengine.
Tags
MICHEZO KITAIFA