Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akifungua kikao cha kujadili
amani katika mkoa wa Arusha ambacho kilifanyika katika bwalo la
Maofisa wa Polisi Arusha (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha)
Meya wa halmashauri ya Jiji la Arusha Calist Lazaro akitoa mchango wake
wakati akichangia mada ya uimarishaji wa amani katika Mkoa wa Arusha
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Sheikh
wa wilaya ya Arusha Abraham Salum akisisitiza jambo wakati akitoa
mchango wake juu ya uimarishaji wa amani katika mkoa wa Arusha ( Picha
na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
……………………………………………………………………………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa
limefanya kikao ambacho kiliwashirikisha viongozi wa dini kutoka
madhehebu mbalimbali pamoja na Madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha
kwa nia ya kuimarisha amani na usalama.
Kikao hicho kilichofanyika jana
katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi kiliwajumuisha watu zaidi
ya mia mbili; Maofisa wa Mkoa wa Jeshi hilo, viongozi wa dini wa
madhehebu yote, Madiwani, Wakaguzi wa Polisi wa Tarafa na Polisi wa
kata.
Akizungumza katika kikao hicho
Kamanda wa Polisi mkoani hapa Naibu Kamishna Charles Mkumbo ambaye
alikuwa mwenyeji wa kikao hicho alifungua kwa kusema kwamba Jeshi la
Polisi pekee haliwezi kukabiliana na uhalifu bali kwa kushirikiana na
viongozi wa dini na wa kisiasa wataweza kuushinda uhalifu.
Alisema makundi hayo ni wadau
wakubwa wa kuimarisha amani kutokana na ushawishi walionao kwa waumini
wao na wananchi wanawaongoza huku Jeshi hilo likiahidi kuwa bega kwa
bega hasa katika upokeaji wa taarifa za uhalifu na kuzifanyia kazi kwa
haraka.
Kamanda Mkumbo alisema kwamba
bila amani hakutakuwa na shughuli zozote za maendeleo ikiwemo uwezekaji
na hata waumini hawataweza kwenda Misikitini na Makanisani kutokana na
hofu ya kiusalama.
“Sote tunajukumu la kufichua
uhalifu na wahalifu kupitia taarifa za waumini wetu hasa kwa viongozi
wetu wa dini kuendelea kuhubiri na kutoa mawaidha katika Makanisa na
Misikiti huku Madiwani waendelee kufanya hivyo katika maeneo yao ya
kiutawala hasa wanapokutana na wananchi kwenye mikutano mbalimbali”.
Alisisitiza Kamanda Mkumbo.
Kwa upande wake Meya wa jiji la
Arusha Calist Lazaro alisema kwamba wananchi pamoja na viongozi wote
wasiwe na hofu kwa kuwa Jiji la Arusha linaongozwa na CHADEMA kwani wao
kama viongozi wa Siasa wanahitaji amani na wanalitambua jukumu hilo na
wataendelea kutoa ushirikiano na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vyote
vya usalama huku akiwataka baadhi ya askari wa Jeshi hilo kufuata haki
katika utendaji wa kazi zao.
Sheikh wa wilaya ya Arusha
Abraham Salum alisema kwamba kikao hicho kimekuja wakati muafaka kwani
mikoa ya Tanga na Mwanza kumejitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani
matukio ambayo hapo awali hayakuwepo katika nchi yetu na kulishauri
jeshi hilo kuongeza weredi katika kupambana na uhalifu huku akiwataka
wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo.
Akichangia mjadala huo Padre
Festus Mangwangi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia, alisema kwamba wao
kama viongozi wa dini wana dhamana kubwa ya kulisaidia Jeshi la Polisi
katika kuhubiri amani kupitia waumini wao. Alisema amani iliyopo
idumishwe kwani baadhi ya nchi zinavurugu na zinatamani amani iliyopo
hapa nchini.
Akihitimisha kikao hicho
kamanda Mkumbo aliwashukuru viongozi wote waliohudhuria kwa michango yao
yenye tija kwa mustakabali wa uimarishaji wa amani ndani ya mkoa wa
Arusha na kusema kwamba ana matumaini makubwa ya kupata ushirikiano toka
kwao naye kuahidi kutatua kero zilizowasilishwa na washiriki ambazo
zipo ndani ya uwezo wake.
Tags
HABARI KITAIFA