Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilla Mkumbo amesema kuna
mambo mawili yanayoibana Serikali katika mgogoro wa wanafunzi
waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Akizungumza
jana kwenye kipindi cha ‘Kipima Joto’ kinachorushwa na kituo cha luninga
cha ITV, Profesa Mkumbo alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama, kwa
sababu ndiyo iliyoanzisha utaratibu wa kudahili wanafunzi wa kidato cha
nne kupitia mfumo maalumu kabla ya kuanza kusoma shahada ya chuo kikuu.
Pia, alisema
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), haiwezi kuhusika moja kwa moja kwenye
udhaifu uliojitokeza katika udahili wa wanafunzi hao, bali Seneti ya
Udom inapaswa kuwajibika katika hilo.
Alisema kuna
udhaifu wa kiutendaji kwa seneti hiyo yenye mamlaka ya kudahili
wanafunzi wenye sifa ambayo iliiacha kazi hiyo mikononi mwa TCU.
Mkumbo alisema kazi ya TCU ni kuidhinisha majina ya wanafunzi waliokwisha dahiliwa na chuo husika na si kuchagua.
“Chuo
chochote ndicho kinachagua wanafunzi wenye sifa wanazozihitaji,
inashangaza kuona Udom imefanyiwa kazi hiyo, baraza na seneti wanapaswa
kuwajibika kwanza, TCU haiwezi kukichagulia chuo wanafunzi,” alisema Profesa Mkumbo.
Hata hivyo,
alitoa angalizo kwa Serikali kutodharau mfumo huo wa udahili kwa
wanafunzi ambao hawakuhitimu Kidato cha Sita kama ilivyoamriwa na
Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa upo na unatumika duniani kote.
“Ila kama
Rais (John) Magufuli hautaki na ameona turudi kwenye mfumo wa zamani
ambao mwanafunzi anapaswa kufaulu kidato cha sita ndiyo ajiunge na chuo
kikuu sawa, lakini atambue kuwa kuna hasara na faida zake, vyuo vingi
vinaweza kufungwa,” alisema Mkumbo
Mbali ya mfumo
huo, profesa huyo alisema upo mfumo mwingine wa udahili kwa mtu yeyote
mwenye umahili katika taaluma yake kusoma shahada kwa kuzingatia vigezo
maalumu vilivyowekwa.
“Ila hakuna jinsi, nadhani TCU wamemsikia Rais kuwa hataki njia za mkato tena.”
Mei 29, Udom
iliwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu
wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni mara
moja.
Amri hiyo
iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, ilisema Serikali imeamua warejee kwao na wataelezwa mustakabali
wao mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo,
Rais John Magufuli juzi alisema baadhi yao walikuwa vilaza, hivyo
wajitafutie mahali pa kwenda huku wenye ufaulu wa daraja la kwanza na
pili aliahaidi kuwa wataandaliwa utaratibu.
Tags
HABARI KITAIFA
