Mkuu wa Kitengo cha Biashara
za Serikalini NMB Bi. Domina Feruzi kulia akimkabidhi mfano wa hundi ya
shilingi milioni 206 Makamu Mwenyekiti wa ALAT Bw. Stephen Mhapa
kushoto kwa ajili ya mkutano wa 32 wa jumuiya hiyo wakati wa mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam.
Makamu Mwenyekiti wa ALAT Bw.
Stephen Mhapa kushoto akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani
kuhusu mkutano wa 32 wa ALAT utakaonza mwishoni mwa Septemba mwaka huu ,
kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikalini Bi. Domina Feruzi.
Picha Na Ally Daud-Maelezo
…………………………………………………………………
Na Ally Daud-Maelezo
Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi katika mkutano mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Nchini
(ALAT) ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi ujao mkoani Musoma.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam Makamu Mwenyekiti wa ALAT Bw. Stephen Mhapa
amesema kuwa, katika mkutano huo wanatarajia Rais Magufuli kuwa mgeni
rasmi ili kufikia malengo ya mkutano huo.
“Tumeamua kumuomba Mheshimiwa Rais
kuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kupata matunda mema ya mkutano huo
kutokana na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu ili kuendana na kasi hiyo
katika kuleta mendeleo na uongozi bora nchini,” alisema Bw. Mhapa.
Aidha Bw. Mhapa amesema kuwa
uzinduzi wa mkutano huo utaendana na ukabidhishaji wa zawadi kwa mshindi
wa shindano la Halmashauri bora kwa mwaka 2016 ambapo mshindi
atayechaguliwa na wananchi kwa wingi atakabidhiwa Trekta yenye thamani
ya shilingi milioni 56 ili kuinua shughuli za kimaendeleo.
Mbali na hayo Bw. Mhapa ameongeza
kuwa mkutano huo utadhaminiwa na Benki ya NMB kwa kupokea kiasi cha
shilingi milioni 206 ambazo milioni 56 zitatumika kugharamia zawadi na
milioni 150 kugharamia mkutano huo.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha
Biashara za Serikalini kutoka benki ya NMB Bi. Domina Feruzi amesema
kuwa wameamua kufadhili mkutano huo ili kurahisisha shughuli za
kimaendeleo na kupata uongozi bora kwa faida ya watanzania.
“Tumeamua kudhamini mkutano huo
ili kuweza kurahisisha shughuli za kimaendeleo na kupata viongozi bora
kwa kupitia mashindano ya Halmashauri Bora mwaka 2016,”amesema Bi.
Domina.
ALAT imekuwa na utaratibu wa kutoa
zawadi kwa Halmashauri bora kwa mwaka wa pili sasa ambapo imesaidia
Halmashauri nyingi kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato na uboreshaji
wa miundo mbinu na mazingira kwa ujumla.
Tags
HABARI KITAIFA