*Asema safari imeiva, ataka wajipange kuhamia Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema safari ya kuhamia Dodoma imeiva na amewataka watumishi wa Ofisi
ya Waziri Mkuu wajipange kisaikolojia.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano,
Agosti 18, 2016) alipokutana na kuzungumza na watumishi wa ofisi yake
kutoka taasisi, idara na vitengo mbalimbali waliopo Dar es Salaam.
Waziri Mkuu aliwataka watumishi
hao watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo
lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha
TANU.
“Tangu wakati huo kumekuwa na
juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya
nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,”
alisema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa
Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa
Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho
ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,”
alisema.
“Napenda kuwatoa hofu, mambo
yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva sasa. Kikubwa ni kwamba
tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,” alisema.
Aliwataka watumishi hao wazidishe
mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya
kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu. “Watumishi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye kazi kwa
bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi na
kinafanikiwa,” alisema.
Tags
HABARI KITAIFA