Mashuhuda wa
ajali iliyosababisha kifo cha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania
(UWT) Mkoa wa Dodoma, Salome Kiwaya wamesema alikufa kutokana na
kushindwa kupewa msaada kwa haraka.
Walisema baada
ya ajali walisikia sauti za watu wakilia kuomba msaada lakini ilichukua
muda wa sasa tatu ndipo walipopata msaada wa kuokolewa kutokana na
ukosefu wa vifaa vya uokoaji.
Juzi katika
eneo la Emmaus mkoani hapa ilitokea ajali ya gari la Toyota Noah na lori
ambayo ilichukua maisha ya Mwenyekiti huyo na watu wengine watatu
kujeruhiwa.
Mmoja wa mashuhuda hao Amri Juma alisema alisikia sauti za wanawake wakiomba msaada ili waweze kuokolewa.
“Ni jambo la
kusikitisha kuona zaidi ya saa tatu hakuna vifaa vya uokoaji
vilivyokuwa vimefika kwa ajili ya uokoaji, ajali ilitokea saa nane
mchana lakini mpaka saa 11 jioni ndio watu wanakuja kutolewa.
‘’‘Breakdown
moja ilipofika ilishindwa kunyanyua lori, ilipofika ya pili ilishindwa,
hali inayoonesha kuna uhaba wa vifaa hivyo mamlaka husika zijipange
kuwa na vifaa vya uokoaji."
Juma alisema
Dodoma imeanza kuandaliwa kuwa makao makuu ya nchi hivyo wakati umefika
wa kuanza kujengewa uwezo wa kuwa na vifaa vya kisasa vya uokoaji.
Katibu wa UWT Mkoa wa Dodoma, Kaundime Kasase, akizungumzia kifo hicho alisema;
“imeniuma
sana na bado inaniuma, sina hata la kusema kwani nimefanya naye kazi kwa
ukaribu, alikuwa mtu anayependa viongozi wake wote."
Mtoto aliyekuwa ndani ya gari hilo, Dearest Mabuba (8) alisema;“Tulikuwa
tumetoka kwenye birthday (siku ya kuzaliwa) yangu ndipo gari likapata
ajali, mama yangu Annastazia Amandus ambaye alikuwa akiendesha gari hilo
akaumia kichwani na dada akachanika kwenye kiwiko,” alisema.
Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffari Mwanyemba alisema wamempoteza mtu muhimu.
“Alikuwa akijichanganya kila mahali, tumepoteza mtu muhimu tuige mazuri yake”.
Mbunge wa Viti Maalumu na Mwenyekiti mstaafu wa UWT Mkoa wa Dodoma, Fatma Tawfiq alisema;
“Mwenyezi Mungu ndiye alikuwa akifahamu siri hii. “Ni jambo la kushtukiza sana tumuombee Mungu amuweke mahali pema peponi,”alisema.
Hata hivyo kwa
upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Dodoma,
Marson Mwakyoma alisema walifika eneo la tukio dakika 10 baada ya ajali
hiyo kutokea.
“Si lazima
askari avae sare tulifika mapema na vikosi vingine vya uokoaji vilikuja
kwa wakati, nadhani kitu muhimu kinachotakiwa kufanyika ni kuimarisha
vifaa vya uokoaji,” alisema.
Tags
HABARI KITAIFA
