Na Baraka Mbolembole
Unaikumbuka game ambayo Ulimboka Mwakingwe alivunjwa mguu na rafiki yake? Ilikuwa Moro United vs Simba SC. Unakumbuka ni mwaka gani? Na nani aliyemvunja mguu? Hakuna siri itakayoachwa ipotee naamini mipango ya Mungu si ya mwanadamu.
Shekhan Rashid alikuwa katika kikosi cha Moro United, Julius Mrope unakumbuka ulipofuatwa nyumbani ili idadi ya wachezaji wanaoruhusiwa ‘kuruhusu mechi ichezwe’ itimie upande wa Moro United. Muda umekwenda sana lakini mechi ile iliharibu maisha ya watu wengi.
Kocha, Athuman Cairo anakumbuka mwaka ule alipokuwa anaombwa na wachezaji wakubwa kama Boniface Pawassa, Idrissa Rajab, Pitchou, Shekhan, Sunday Peter, Ally Yusuph Tigana kujumuika na sisi Jamaica katika mazoezi.
King Kibadeni nilikuwa namuhurumia…
Kwa vile wao Moro hawakuwa na uwanja wa mazoezi na pale Morogoro, Sekondari ulikuwa uwanja maalum wa Polisi Moro FC na Jamaica FC iliwabidi wawahi mapema mchana wa jua kali kufanya mazoezi na wachezaji wasiozidi 12.
Nilishangaa sana, kwa maana Moro United ilikuwa ikifahamika kama ‘Chelsea ya Bongo’ na mwaka mmoja nyuma ilishindwa kushinda ubingwa licha ya kushinda game 15 za mzunguko wa kwanza VPL. Mimi ni shabiki mkubwa wa Pawassa, pia nilikuwa napenda sana juhudi za Idrissa Rajab.
Heshima na mapenzi ya soka nilijifunza kutoka kwa Shekhan, Pitchou, Steven Mazanda na nilishangazwa na mengi kuhusu Tigana ambaye wakati nakua mara nyingi watu walimuandika vibaya. Hawa jamaa wanaupenda sana mpira na siku ya kwanza mazoezini kucheza na Pawassa na Idrissa kama wachezaji watatu wa safu ya kati ya ulinzi.
Baada ya dakika kadhaa, Pawassa akaniambia, “unacheza vizuri sana, jitahidi kufanya mazoezi.” Baadae Idrissa naye akaniambia maneno ya kunitia moyo. Ila mimi nilikuwa naona raha kucheza na wachezaji hao japo katika mazoezi tu, na nilihitaji kuwauliza kwanini wapo wachache sana katika timu yao wakati wapo katika ligi.
Nilitaka kuwauliza ‘hawachoki’ kwa maana mimi nilikuwa nawahi mapema uwanjani kuwatazama mazoezi yao, kisha Polisi Moro ambao walikuwa wakianza mida ya saa 9 au 9.30, halafu sisi Jamaica mida ya saa 11.
Ila nilisita, lakini tayari nilifahamu ndani ya Moro United kulikuwa na ukata mkali. Nimeelezea haya yote lakini si hoja yangu.
Dau ambalo lilimvunja mguu, Ulimboka lilikuwa ni 500, 000 (laki tano). Kuna mtu kabla ya mechi kuanza alininong’oneza, “Pawassa atakula red…”
Kumbuka wakati huo Simba haikuwa na rekodi ya kuishinda Moro United pale Morogoro na ili wapate nafasi moja kati ya nafasi mbili za juu katika ligi walipaswa kuishinda timu hiyo ‘iliyopotea.’
Dakika chache baada ya kuanza kwa mechi, Pawassa akacheza rafu ya makusudi akapewa kadi ya njano. Siku hiyo kiungo mshambuliaji wa Moro United, Sunday Peter alipangwa katika beki namba mbili kwa sababu timu yake ilikuwa imekimbiwa na wachezaji wengi wakati ligi ikiendelea, na katika benchi la wachezaji wa akiba kulikuwa na mchezaji mmoja tu.
Moro walikuwa wababe wa Simba na uongozi wa timu hiyo ya Dar es Salaam wakati huo uliamua kumtumia mchezaji wao wa zamani ili kupata matokeo. Wakati, Ulimboka akikimbilia mpira katika upande wa kushoto, Pawassa ambaye alikuwa beki wa kati, naye akatoka mbio.
Wote pale uwanjani tulitegemea mlinzi huyo wa zamani wa Simba, APR na timu ya Taifa ya Tanzania angeenda kuucheza mpira ule lakini maajabu akamrukia Ulimboka na kucheza faulo ambayo ilikuwa ya wazi na licha ya kuwa na kadi ya njano faulo ile ya Pawassa dhidi ya Ulimboka ilistahili red ya moja kwa moja.
Ulimboka, masikini akavunjwa mguu na rafiki yake mwenyewe na mpango ambao ulipangwa ukageuka na kuwa ‘sumu’ ambayo ilimtafutana Pawassa katika maisha yake ya soka na kumaliza kipaji cha aina yake cha Ulimboka.
“Umeamini kile nilichosema kabla ya kuanza kwa mechi?” akaniuliza yule mtu ambaye awali aliniambia, Pawassa amepewa kitu kidogo ili apate red card kwa malengo ya kuidhohofisha Moro United ili Simba ipate matokeo ya ushindi.
Walifanya vile kwa kuamini mtu pekee ambaye ni kikwazo kwao (Simba) kupata matokeo ni Pawassa kwa maana Moro haikuwa na beki mwingine katika benchi wala ndani ya uwanja.
Tigana akafunga goli la uongozi upande wa Moro United licha ya kubaki pungufu uwanjani na Simba walipambana sana na baadae wakasawazisha na dakika za mwisho wakapata goli la ushindi. Game ikamalizika kwa matokeo ya Moro United 1-2 Simba.
Mashabiki wa Simba walipopata taarifa kuwa Ulimboka amevunjika mguu wakaanza kumlaumu Pawassa.
Uli, alikuwa staa na mchezaji wa ukweli katika kikosi cha Simba wakati ule na kuvunjwa mguu halikuwa lengo bali ilitokea kama bahati mbaya tu. Malengo yalikuwa Pawassa apate kadi nyekundu na Moro United idhohofike ili Simba wapate matokeo.
Ilikuwa mwaka 2006, takribani miaka kumi sasa imepita. Sehemu ya makubaliano ilikuwa ni kumrudisha Simba mlinzi huyo lakini wakamgeuka na kumuacha mtaani baada ya kupata walichotaka na kumpoteza Ulimboka.
Achana na tukio lile la kukamatwa kwa Ulimboka kwa madai alijaribu kutaka kumpa hongo mlinda mlango wa Mtibwa Sugar wakati huo, Shaaban Kado.
Na waliyapata lakini walipata na hasara kumpoteza mchezaji wao bora katika timu. Soka la Tanzania litachukua muda mrefu kusimama kwa kuwa matokeo mengi yanapangwa nje ya uwanja, wachezaji wanapewa rushwa ili kuzifungisha timu zao.
Watawafungia waamuzi kila mwaka lakini mambo hayatabadilika kamwe.
Tags
MICHEZO KITAIFA