WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote
za Serikali mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la sh. bilioni 1.4
zikiwa ni bili zao za maji.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati
akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dodoma (DUWASA) mara baada ya kukagua utendaji kazi wa chanzo cha
maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa Dodoma.
“Niletee
haraka orodha ya wadaiwa wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma
ambao hawajalipa bili zao. Madeni yote ni lazima yalipwe,” amesema
Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu
ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya
Serikali kuhamia Dodoma, anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma
za jamii pamoja na kukagua miundombinu ya mkoa huo.
Aliutaka
uongozi wa DUWASA na watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za
upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi
au wawekezaji wanaponunua viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze
ujenzi mara moja.
“Tumealika
wawekezaji, nataka wajenge viwanda na mahoteli hapa Dodoma, sasa
wakikuta maji na umeme kwenye maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha
kuharakisha kazi za ujenzi,” amesema.
Pia
amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bi. Christina Mndeme ahakikishe
eneo lililo jirani na chanzo hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na
linalindwa dhidi ya uchomaji mioto.
“Uchomaji
moto uoto wa asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa
nchini na halina budi kusimamiwa hadi liishe,” amesisistiza.
Amefikia
uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
DUWASA, Mhandisi David Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza kujenga
na kufanya shughuli za kijamii jirani na chanzo hicho licha ya kuwa
walikwishaondolewa zamani.
Kuhusu
wadaiwa sugu, Mhandisi Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za
Serikali ndiyo wanaongoza kwa kulimbikiza madeni. “Wananchi wa kawaida
wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo kubwa na hao tunawamudu,” alisema
wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema
changamoto nyingine inayowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi karibuni
uliwashwa moto na kuunguza baadhi ya nguzo za umeme ambazo zinapeleka
umeme kwenye chanzo hicho.
Alisema askari wa JKT Makutupora walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya chanzo hicho cha maji.
Waziri Mkuu
pia alikagua maabara ya upimaji maji kwenye chanzo hicho kabla
hayajasambazwa kwa wateja na mara yanapokuwa yamefika kwa wateja na
kuelezwa kuwa maji hayo yanakidhi viwango vya kitaifa na vya kimataifa
vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha magodoro Dodoma na kituo cha kuzalisha umeme cha Zuzu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, OKTOBA 2, 2016
Tags
HABARI KITAIFA