BANDA MEDIA BLOG

Jicho la 3: Jicho langu la 3, litaona vibaya ila halitakosea katika Simba SC hii ya Rage, Aveva, Kaburu na Zacharia Hans Poppe

Zacharia Hans Poppe, mwenyekiti wa kamati ya usajili Simba SC
Na Baraka Mbolembole
Kitu muhimu katika maisha ni uhai, muda ni jambo maalumu. Katika mipango ya mafanikio uvumilivu ni jambo la kipekee, hekima na busara.

Ulimsikiliza mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa Simba SC, Zacharia Hans Poppe? Hawa ndiyo mabosi wenye mpira wa Tanzania, ambao hupewa majukumu hayo kutokana na ushawishi mkubwa wa pesa!
Hawa ndiyo watu wa mpira waliopo katika soka la Tanzania. Kitu kikubwa alichoniachia Aden Rage katika miaka yake minne ya uenyekiti wa Simba ni pale alipoamua kuwaambia walimwengu kwa msisitizo kuwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ambao pengine labda walimpigia kura katika uchaguzi uliomwingiza madarakani yeye kama mwenyekiti na Geofrey Nyange Kaburu kama makamu mwenyeki katikati ya mwaka 2010 ni ‘MBUMBUMBU.’
Kama haujui maana yake nenda katika kamusi utaelewa vizuri alikuwa na maana gani. Niliona ‘anguko’ la Rage mara baada ya kushindwa katika jaribio lake ‘hewa’ la kumzuia mlinzi wa kati Kelvin Yondan na ‘danganya-toto’ aliyowafanyia baadhi ya wanachama waliokuwa na hasira na yeye.
Agosti, 2012 katika mkutano wa mwaka wa klabu ya Simba, Rage akiwa mwenyekiti, Kaburu kama makamu mwenyekiti na Poppe akiwa katika nafasi aliyopo sasa, Rage aliwaambia wanachama wake kwamba anashindwa kuendeleza mchakato wa ahadi yake ya kuisaidia Simba kumiliki uwanja wake binafsi ndani ya utawala wake kutokana na timu hiyo kushindwa kuwa na kiasi cha milioni 30 ili kulipia hati ya umiliki wa kiwanja cha Bunju.
Rage alikuwa ‘mwanasiasa’ na licha ya kushinda kikatiba mara kadhaa katika majaribio ya kupinduliwa kwake na wajumbe wa kamati ya utendaji, Rage hakuwa kiongozi mbaya, lakini ahadi yake ya uwanja ilimuangusha vibaya.
Simba 5-0 Yanga SC, Mei 2012 ni rekodi ‘bab-kubwa’ lakini anguko la Simba lilianzia pale, huku mijadala kuhusu milioni 300 za uhamisho wa Mbwana Samatta na Mganda, Patrick Ochan, Mei, 2011 kwenda TP Mazembe iliyumbisha uhusiano wake na baadhi ya wanachama.
Simba kukosa milioni 30, Mei, 2012 ili kuongezea katika milioni 50 iliyotajwa kuwepo mwaka mmoja baada ya Samatta na Ochan kuuzwa ilikuwa sababu ya kisiasa zaidi, na ‘watu masikini’ hawakupata kuhoji chochote baada ya kupitishwa kwa ‘harambee’ na kupatikana kiasi cha milioni 32 na ushee hivi.
Teh teh teh, acha muendelee kuisoma namba. Mr.Kazi Nyingi akachangia milioni 10, mwenyekiti akachangia milioni 5, makamu mwenyekiti pia akachangia milioni 5. ‘Watu masikini’ bhana, yaani wakashangilia kabisa.
Kila media wakaitawala wao kwa tambo. Mambo yakaenda kama nilivyotaka yaende, ndani ya misimu miwili ya mwisho ya Rage timu ilimaliza nafasi ya tatu na ile ya nne.
Baada ya kujipima, yeye mwenyewe akasema hatogombea nafasi yoyote katika uchaguzi wa Juni, 2014 ambao ulimuingiza madarakani, Avance Aveva kama rais wa klabu na Kaburu kama makamu wa rais, huku Poppe akibakizwa kama mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Nakumbuka wakati wa kampeni zake kuelekea mkutano wake mkuu wa uchaguzi June, 2014, Aveva aliamini katika sera ya ‘pointi 3’ na aliyeonekana mpinzani wake mkuu, yeye aliamini zaidi katika maendeleo ya klabu kiuchumi na kimpira hata kama hawatashinda mataji wakati wake wote wa utawala.
Kuna baadhi ya watu wanaamini Wakili, Damas Ndumbaro ni mtu muhimu katika mpira wa Tanzania, lakini wakati mwingine huwa simuonei huruma huko alipotupwa na watawala wa sasa soka la Tanzania ambao pengine baadhi aliwasaidia kuwa katika nafasi zao sasa.
Ndumbaro hakuwahi kuitendea haki Simba SC baada ya kuondoa jina la Michael Wambura na kuwafanya wanachama wengi kumpigia kura, Aveva pekee kwa maana mpinzani wake mkuu aliondolewa ‘kimizengwe’ tu.
Nikasema, baada ya miaka miwili bila taji la ligi kuu chini ya utawala wa Rage, niliandika, miaka mingine minne inafuata. Na nitaendelea kuamini hivyo maana umakini wa watawala wa klabu hiyo ni mdogo, huku baadhi ya wanachama ‘wakiwa ni bendera, fuata upepo.’
Hawajui hata timu yao ilipotoka, inapopita na hawana tafakari ya kule inapokwenda. Napenda kumuita Poppe jina la Mr.Kazi Nyingi kwa sababu majuzi nimemsikia mahali akisema, “Tunajenga upya timu yetu…” Labda niwaambie tu, Mbuyu Twite na Yondan wapo Yanga hadi sasa wakishinda mataji.
Mliaminishwa na Rage kuwa ni wachezaji halali wa Simba. Mrisho Ngassa pia alitoka Simba na kucheza Yanga ‘kijeshi-jeshi,’ Hassan Kessy anaenda kushinda VPL akiwa Yanga, na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ anaweza kuwaacha hivi, kama ilivyokuwa kwa Ramadhani Singano.
Nilikuwa nikiwashangaa sana waliokuwa wakipiga kelele kusema Simba itashinda VPL, tena hadi kocha wao, Joseph Omog alisisitiza watafanya hivyo bila kupoteza mchezo.
Vipigo viwili tu, mfarakano mkubwa! Simba SC Tafuteni busara ilipo ili mfanikiwe, kama Hajji Manara ndiye msemaji wa klabu, mpeni nafasi yake.
Sasa yale ni maneno gani kwa wachezaji, tena yakisemwa katika media na kiongozi mkubwa.
Mtu mkubwa ni mwanafunzi. Mafionso…! Jicho langu la 3 bado lilishaona miaka 6 mfululizo ya Simba SC bila VPL, na bado linaendelea kuona sababu muhimu za kuanguka kwa timu hiyo sababu ya Rage, Aveva, Kaburu na Poppe, mnaoamini mafanikio chini ya watu hao endeleni kuamini, mimi naendelea kuisoma namba ya Simba bila VPL nisaidieni jina la yule kijana wa African Lyon aliyemtungua yule kipa bora wa Simba.
Victor Hangaya naendelea kumtafuta, punde ataniambia alipewa kiasi gani kuharibu kibarua cha Vicent Angban.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG