Na Athumani Adam
Ligi kuu nchini England iliendea mwishoni mwa juma kwa mechi za raundi ya kumi na moja kuchezwa kwenye viwanja mbali mbali. Siku ya Jumamosi Chelsea iliongoza ligi kwa muda baada ya kufikisha pointi ishirini na tano pale ilipopata ushindi wa 5-0 dhidi ya Everton.
Ushindi wa Liverpool siku ya Jumapili dhidi ya Watford wa mabao 6-1 umeifanya Liverpool kuitoa Chelsea kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 26.
Mbali na matokeo kuna takwimu mbali mbali zilizoandikwa baada ya michezo ya wikiendi hii. Makala hii inakupa takwimu hizo muhimu katika mtindo wa namba;
Namba 25,000 (Zlatan Ibrahimovic)
Baada ya kupita mwezi October bila ya mshambuliaji wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovi kufunga bao kwenye ligi kuu siku ya Jumapili alifanikiwa kutikisa nyavu mara mbili kwenye ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Swansea City.
Bao la Zlatan limemfanya kuwa mchezaji aliyefunga bao la 25000 tangu kuanzishwa kwa ligi kuu nchini England.
Namba 139 (Arsenal Vs Tottenham Hotspurs)
Kwenye mechi ya watani wa jadi kutoka Kaskazini mwa jiji la London, Arsenal dhidi ya Spurs kwenye uwanja wa Emirate mabao mawili yalifungwa na mchezo kuisha kwa sare ya 1-1.
Mabao hayo mawili yamefanya mechi ya Arsenal dhidi ya Spurs kufikisha mabao 139 pindi timu hizo zinapokutana ikiwa ni mabao mengi zaidi baina ya timu mbili kwenye ligi kuu England.
Namba 23 (Eden Hazard)
Everton walikubali tena kuwa wateja wa Chelsea kwenye dimba la Stamford bridge baada ya kupoteza kwa mabao 5-0. Bao la pili la Hazard lilikuwa la kusimimua, Chelsea walitengeneza bao hilo kwa kupiga pasi 23 kabla ya Hazard kufunga.
Namba 9 (Manchester city)
Manchester city walishindwa kuibuka na pointi tatu dhidi ya Middlesbrough baada ya kukubali sare ya 1-1 kwenye dakika za majeruhi siku ya Jumamosi. Bao ambalo City walifungwa na Middlesbrough limeifanya City kucheza mechi tisa bila kuzuia nyavu zao kutikiswa (Clean Sheet).
Namba 5 (Mauricio Pochettino, Saido Mane, Adam Lallana)
Sare ya Tottenham dhidi ya Arsenal imemfanya kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino kuwa kocha pekee wa Spurs aliyeweza kuingoza timu yake kufikisha mechi tano kwenye pambano la watani wa jadi Kaskazini mwa London (North London Derby) bila kupoteza.
Mabao mawili ya Mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane kwenye mchezo dhidi ya Watford ambapo Liverpool ilishinda kwa 6-1 umemfanya Mane kufikisha mabao matano kwenye mechi tano ndani ya uwanja wa Anfield.
Kiungo wa Liverpool Adam Lallana amefikisha pasi tano za mabao msimu huu, mchezaji pekee aliyetoa pasi nyingi hadi sasa ni Kevin De Bruyne mwenye pasi sita.
Namba 3 (Manchester City)
Sare ya Man City dhidi ya Middlesbrough imekuwa ni sare ya tatu mfululizo kwa City kwenye dimba lao la nyumbani, Etihad Stadium. Mara ya mwisho kwa City kushuhudia sare tatu mfululizo ilikuwa November 2009 chini ya Kocha Mark Hughes.
Tags
MICHEZO KIMATAIFA