Makamu mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya MOI Prof Bakari Lembariti akihutubia wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi wa MOI wakati wa Uzinduzi wa Kikao cha Tatu cha Baraza Hilo
Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman Kiloloma akiwasilisha ripoti ya Utendaji ya Mwaka 2015/2016
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa MOI wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Prof Bakari Lembariti
Makamu mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi MOI Prof Bakari Lembariti akimkabidhi cheti Mfanyakazi bora
wa MOI kwa Mwaka 2015/2016 Bwana Robert Sere
…………………………………………………………………
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya MOI Profesa Bakari Lembariti leo amezindua vikao vya Baraza
la Tatu la Wafanyakazi wa MOI katika ukumbi wa IDDI NYUNDO katika
halmashauri ya Temeke jijini Dar es Salaam. Vikao vimehudhuriwa na
zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika kila idara, vitengo na chama cha
wafanyakazi wa MOI (TUGHE) na wajumbe wa TUGHE mkoa.
Akizindua Baraza hilo Profesa
Lembariti alisema anampongeza Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli. Alisema ” Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi
ya wadhamini MOI Mh Zakia Meghji natumia Fursa hii kumshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uongozi wake
uliotukuka na jitihada zake za kuboresha huduma za afya hapa nchini,
sote ni mashahidi“.
Aidha, Profesa Lembariti
aliwakumbusha wafanyakazi wa MOI kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia
maadili ya utumishi wa Umma ili kujenga imani kwa watanzania walio wengi
ambao wanaitegemea MOI kama Taasisi pekee inayotoa Tiba ya kiwango cha
juu cha rufaa kwenye Tiba ya Mifupa, upasuaji wa ubongo na mishipa ya
fahamu.
Pia Profesa Lembariti alisema ni
vyema wajumbe wa Baraza la MOI wakatumia vikao vya Baraza kujadili
changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi ya MOI na kutafuta
muarobaini ili Taasisi ya MOI iendelee kutoa huduma bora
Kwa upande mwingine Profesa
Lembariti aliwakabidhi zawadi wafanyakazi Bora wa MOI kwa mwaka
2015/2016 ambapo Bwana Robert Sere aliibuka kidedea na kuwa mfanyakazi
Bora wa MOI na kujipatia cheti na fedha taslimu kiasi cha Tshs Milioni
4, nafasi ya pili ikishikwa na Bwana Lucas Machage akijipatia cheti na
kiasi cha Tshs Milioni 2 na nafasi ya tatu ikishikwa na Bi Betty Shila
ambaye alijipatia cheti na kiasi cha Tshs Milioni 1.5
Kwa upande wake ,akiwasilisha
ripoti ya utendaji wa Taasisi ya Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman
Kiloloma alisema kutokana na ongezeko kubwa la ajali ambazo zimepelekea
ongezeko kubwa la wagonjwa MOI, Taasisi ya MOI iko kwenye mpango mkakati
kabambe wa kushirikiana na baadhi ya hospitali za rufaa za pembezoni
kwa kuwapeleka wataalamu kutoa huduma katika hospitali hizo na kupunguza
kama si kuondoa kabisa wimbi la wagonjwa wanaopokelewa MOI
Dkt Kiloloma alisema kwamba
Taasisi ya MOI imeendelea kuwa Kitovu cha Weledi katika matibabu ya
Mifupa ,Ajali ,Ubongo na Mishipa ya Fahamu katika ukanda huu wa Afrika
Mashariki na kati ambapo mwaka 2015 MOI ilitoa utafiti bora wa mfupa
mrefu wa paja duniani ,ambapo utafiti uliwasilishwa katika Taasisi ya
kimataifa ya upasuaji wa mifupa duniani ya Marekani (AOTA)
Vilevile, Dkt Kiloloma aliwaomba
wajumbe wa Baraza la MOI kutoa michango yenye tija ili kupata matibabu
ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi ili Taasisi iendelee
kutoa huduma bora kwa watanzania
Tags
HABARI KITAIFA