Huyu ni Rafiki yangu toka udogo,tukiwa shule ya Msingi mpaka
Sekondari.Tulikaa pamoja na kusoma pamoja.Namzungumzia rafiki wa kufa na
kuzikana.
Duniani kuna visa wakuu,visa hivi visikie kwa jirani lakini visikukute
wewe au mtu wako wa karibu.Miaka 10 iliyopita,mwezi kama huu,huyu ndugu
yangu alianza taratibu za kukata rufaa ili shauri lake liweze
kusikilizwa tena.
Alifungwa kifungo cha miaka 30 gerezani.Kesi yake ilikuwa ya kutungwa na
kubambikiwa.Pesa ilitembea na wakubwa wakaisimamia kesi yake.Nakumbuka
alivyolia kwa kilio cha nguvu,siku Jaji alipogonga meza baada ya
kumuhukumu kutumikia miaka 30 behind the bars!!
Kosa la kusingiziwa kubaka lisikie tu,kweli sio wote walio garezani wana hatia,wengine ni kesi za kusingiziwa.
Kila nilipoenda kumcheki gerezani jamaa alikuwa analia sana.Aliamua kuwa
muhubiri na mwimba kwaya wa gerezani,katekista na muongoza ibada
mbalimbali mle gerezani.Aliamini ipo siku atatoka,maana alimlilia Mungu
wake,toka mawio ya jua mpaka machweo yake.
Baada ya miongozo ya watu wa gerezani(Wafungwa wengi hujua sana taratibu
za sheria na namna ya kukata rufaa) jamaa aliamua kukata rufaa.Hoja
kubwa ikiwa,siku na tarehe aliyoshutumiwa kutenda kosa,ndio siku na
tarehe aliyokuwa Dsm,eneo la baraza la Mitihani akifuatilia "result
slip" yake.
Huu ndio ulikuwa ushahidi mkubwa,kitabu cha wageni cha baraza la
mtihani,kilionyesha mnamo terehe hiyo,siku hiyo,majira fulani mshitakiwa
aliandika jina lake na sahihi yake ktk kitabu cha wageni kwenye lango
la Baraza la Mitihani-Dsm.
Kitabu kile kilithibitishwa na Baraza la Mitihani kuwa ni sahihi,na
baraza likathibitisha kuwa,tarehe tajwa,na siku tajwa ya mwezi
tajwa,majira ya mchana,kitabu kinachoonyesha kuidhinishwa na kutolewa
kwa "result slip" kilikuwa na sahihi ya afisa wa NECTA na mchukuaji wa
"result slip" ambaye ndio mtuhumiwa.
Ndugu mwema alishinda kesi,sahihi na jina ktk vitabu vya NECTA vilmuokoa
kuendelea kutumia miaka 29 iliyobaki baada ya kuwa tayari ametumikia
mwaka mmoja jela.Ilikuwa ni siku ya ajabu,ikawa kama ndoto,ilikuwa ni
siku ambayo majina na utukufu wote wa Mungu ulitajwa.Siku hii,kwa sahibu
wangu,haikuhitaji muujiza wa kuhamisha mlima toka uwanda mmoja kwenda
mwingine.Rufaa ile iliyoambataba na ushindi,ulikuwa ni muujiza tosha.
Pesa hudunisha utu,pesa hununua haki na pesa hubadili haki kuwa batili
na batili kuwa haki.Sio wote walio gerezani wana hatia,na sio wote
hawana hatia.
Sasa ni baba wa watoto watatu,ni miaka kumi na ushee sasa imepita.Kama
ilivyo kwa wengine kukumbuka siku yao ya kuzaliwa,kwa ndugu yangu hii
ndio siku kubwa ya kukumbukwa maishani mwake.Kila ifikapo,huandaa ibada
na sadaka...Kumwambia Mungu...WEWE NI MUNGU WA HAKI.
Imebaki kuwa simulizi,itakuwa historia na baadae hadithi.Kimoja na
kikubwa,huwa hatamani kuisimulia hii kwa mke wake,na hadhani kama
atakuja kuisema kwa watoto wake.Imebaki kuwa fundo la siri katikati ya
mifupa ya kifua chake.
Hii ni habari ya rafiki kipenzi,mjelajela wa kubaka!Ambaye hata kwa uso
na sura yake,hudhani kuwa anaweza kutamani kubaka, achilia mbali hata
kubaka kwenyewe.Haki mbinguni,duniani ni ubatili.
Tags
HABARI KITAIFA
