
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema
kwa sasa hatazungumzia kuondolewa kwake kutoka kwenye nafasi hiyo
lakini amesisitiza kuwa “ukweli utabaki kuwa ukweli”.
Katika mazungumzo yake mafupi na Raia Mwema yaliyofanyika juzi Jumatatu,
Muhongo aliwataka Watanzania watulie hadi pale ukweli utakapokuja
kujidhihiri na kwamba yeye hana la kusema kwa sasa.
“Ahsante sana ndugu yangu kwa kunitafuta. Huwezi kupata lolote kutoka
kwangu kwa sababu sitaki malumbano ila ukweli utabaki kuwa ukweli. Mimi
sitaki malumbano ya aina yoyote,” alisema Muhongo.
Katika mazungumzo hayo, msomi huyo hakutaka kufafanua kuhusu ukweli huo ambao anaamini utabaki kuwa ukweli.
Profesa Muhongo, mmoja wa wasomi wabobezi katika masuala ya miamba
duniani, alijiuzulu wadhifa wake huo wiki iliyopita, baada ya Rais John
Magufuli kumtaka ajitathmini baada ya kutolewa kwa ripoti ya Kamati ya
Profesa Abdulkarim Mruma.
Kamati ya Mruma ilipewa kazi ya kuchunguza makinikia yaliyokuwepo
katika makontena yaliyozuiwa kusafirishwa kutoka nchini na kwenda nchi
za nje kwa ajili ya kufanyiwa uchenjuaji.
Baada ya uchunguzi huo wa takribani miezi miwili, kamati hiyo ilibaini
kwamba makinikia hayo yalikuwa na madini ya dhahabu ya takribani tani 15
ambazo serikali ingeweza kupata mrabaha wenye thamani ya hadi shilingi
trilioni 1.4.
Matokeo ya uchunguzi huo uliohusisha makontena 277 ya makinikia ndiyo
yaliosababisha Rais Magufuli kutamka hadharani kwamba Muhongo anapaswa
kujitathmini kama bado anafaa kuwa waziri na ikiwezekana ajiuzulu.
Barua ya kujiuzulu
Hata hivyo, jioni ya siku hiyo, Ikulu ilitoa taarifa ya Ikulu kutengua
uteuzi wa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini; lakini baada ya
taarifa hiyo – takribani saa moja baadaye, mitandao ya kijamii
ilisambaziwa barua ya kujiuzulu kwa Muhongo.
Katika barua hiyo, Muhongo hakukiri makosa yoyote katika jambo hilo
lakini alieleza kwamba alitekeleza wajibu wake wote kama ambavyo
alielekezwa na Rais Magufuli.
“Mheshimiwa Rais, napenda kukufahamisha kwamba nimejitahidi kufanya kazi
kwa uwezo wangu wote kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini tangu
uliponiteua kuwa Waziri mnamo Desemba 12, 2015. Nakushukuru sana kwa
miongozo yako ya kazi ambayo imenisaidia sana katika utekelezaji wa
majukumu yangu ya kazi,” ilieleza barua hiyo iliyoandikwa Mei 24, 2017.
Baadhi ya wanasheria walioiona barua hiyo kupitia mitandao ya kijamii,
walitafsiri maelezo hayo ya Muhongo kama ya kutokubali kukosea lolote
isipokuwa kukubaliana na mamlaka ya uteuzi iliyomtaka aachie ngazi.
Wakati huo huo, wanasheria mashuhuri nchini wamesema huu ni wakati wa
kumsaidia Rais Magufuli na serikali yake katika kuhakikisha kwamba
utajiri wa maliasili uliopo Tanzania unanufaisha nchi na si mataifa
yaliyowekeza hapa nchini.
Wanasheria hao wameonya kwamba Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa
ambayo kama haitaangaliwa vema, huenda taifa likapata hasara kubwa
badala ya faida inayotarajiwa.
Makamu Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi,
alisema suala alilolianzisha Magufuli la kupigania rasilimali za taifa
halina vyama wala itikadi isipokuwa ni la kitaifa.
“Kwa maoni yangu, ningependekeza iundwe sasa tume ya wataalamu
itakayojumuisha watu kutoka serikali ya Tanzania na kampuni za madini
zilizopo nchini ili kwanza ukweli huu uwekwe wazi, baada ya hapo itakuwa
rahisi kwetu kushitaki kwenye vyombo husika,” alisema Ngwilimi.
Kauli hiyo ya Ngwilimi iliungwa mkono na mmoja wa wanasheria maarufu
nchini, Dk. Adelatus Kilangi, aliyesema kwamba kwa hali ilivyo sasa kwa
kuzingatia mikataba ambayo Tanzania imeingia kimataifa, hatuwezi kuvunja
mikataba ya madini iliyopo sasa kwa sababu ya ripoti ya Mruma.
“Hatuwezi kuivunja. Tumesaini mkataba wa MIGA na wa ICSID. Tutashtakiwa
kwa kuvunja Customary Law Principle ya 'Fair and Equitable Treatment',
na 'State Responsibility' na ya 'Respect for Acquired Rights'.
Tutapelekwa mbele ya ICSID na kuhukumiwa, kisha tutaminywa na MIGA
itakayokamata mali zetu popote zilipo.
“Kuwashtaki makampuni kwa kutudanganya? Tunaweza, na tutatumia hoja kuwa
wamevunja Customary Law Principle ya 'Good Faith and Prohibition of
Abuse of Rights'. Lakini wakisema uchunguzi wa mchanga tumeufanya kwa
upande mmoja wanaweza kushinda. Ndiyo maana ni muhimu tufanye uchunguzi
wa pamoja,” alisema Kilangi.
Katika andishi lake aliloliandika kwa jumuiya ya wanafunzi waliowahi
kusoma katika Shule ya Sekondari ya Sengerema na ambalo baadaye
lilisambazwa katika makundi mbalimbali ya WhatsApp hapa nchini, Kilagi
alieleza kwa kina kuhusu changamoto za kisheria, kodi na utawala
zilivyochangia nchi kufika ilipo sasa.
Kwa mfano, alisema ni wazi kuwa wakati nchi ikiingia kusaini baadhi ya
mikataba ya rasilimali, taifa lilikuwa limetekwa na vikundi maslahi
ambavyo vilikuwa vikifikiri kwa niaba ya serikali.
“Kuna tatizo kubwa sana linalozikumba hasa nchi za Afrika na baadhi ya
zinazoendelea zilizo nje ya Afrika. Hili ni tatizo la 'state capture'
(nchi kutekwa na vikundi maslahi). Kama ilivyo concept ya 'river
capture' kwenye somo la jiografia, basi state capture linamaanisha
ushawishi unaofanywa na watu wa kada ya juu, wafanyabiashara au
wawekezaji kiasi kwamba serikali inashindwa kufikiri na kuachia kundi
hilo kufikiri kwa niaba yake.
“Wakati wa kufuata falsafa ya soko huria katika rasilimali, Tanzania
iliingia kwenye utekwaji huu. Ndio kusema tuliondoa kichwa chetu
tukaweka kichwa kingine. Tukawa tunafikiri kwa mfumo wa hicho kichwa
kingine. Sasa tumeanza kurudisha kichwa chetu,” alisema.
Tanzania ilivyobanwa
Katika andishi lake hilo refu, Dk. Kilangi alieleza namna Tanzania
ilivyozidiwa akili katika hatua za mwanzo za kuingia katika mikataba ya
nishati na madini.
Kwa mfano, alitoa mfano wa madini ambapo wawekezaji walikataa kuweka
sheria inayoruhusu nchi inayoibiwa utajiri wake kuomba kupitiwa upya kwa
mikataba endapo kutakuwa na udanganyifu.
“Ili uweze kufanya mapitio ya mikataba, ni lazima kwenye mikataba
tuliyoingia tuwe na kipengele kinachohusiana na doctrine ya 'clausula
rebus sic stantibus. Hiki ni kipengele kinachoruhusu kupitia upya
mikataba kama mambo fulani yakibadilika.
“Lazima kifungu hiki kiwe kwenye mikataba. Hawa jamaa (wenye kampuni za
madini) walihakikisha hakimo kwenye mikataba yetu. Kwa hiyo, ukianza
mchakato wa kupitia mikataba mwenyewe bila ya kuwashirikisha wao
watasema umevunja kanuni ya 'fair and equitable treatment'. Hivi ndivyo
ilivyo,” aliandika mwanasheria huyo.
Kwa mujibu wa msomi huyo, tatizo hilo la kwenye madini lipo pia kwenye
sekta ya nishati, ambapo wenye kampuni huwa tayari kuidanganya nchi kwa
misaada wanayojua inahitajika sana; ikiwamo misaada ya wataalamu, lakini
kumbe wanatengenezea sheria itakayowezesha kutuibia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa
Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk. Rugemeleza Nshala, alisema Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010 na mabadiliko yaliyofanyika mwaka 2015
ilitengenezwa kwa kufuata matakwa ya Benki ya Dunia (WB) na kampuni za
madini zilizopo nchini.
Alisema kuna haja ya kufanya mapitio ya mikataba yote ambayo serikali
iliingia na wawekezaji katika eneo la rasilimali kwa vile ilipitishwa na
watendaji waliokuwa hawajui thamani ya madini hayo.
Nshala alishauri upitiaji wa sheria hii ujumuishe taasisi na wadau wote
wa ndani ya nchi na iandikwe na Watanzania wenyewe na serikali ikatae
msaada wa uandikaji wa muswada wa sheria hiyo kutoka Benki ya Dunia au
mataifa yaliyoendelea kwa kuwa ajenda yao ni kuwa kampuni za nje ndizo
zenye haki ya kuchimba na kunufaika na madini ya nchi husika.
“Uchimbaji na uchenjuaji wa Tanzanite pamoja na utengenezaji wa bidhaa
za mwisho za madini hayo lazima ufanyike Tanzania. Kampuni kama Tiffany
ziambiwe kuwa ni lazima waanzishe viwanda vya utengenezaji vito na
mapambo yatokanayo na Tanzanite nchini. Hivyo nchi yetu ndiyo iwe duka
la bidhaa za Tanzanite na si Marekani kama ilivyo sasa,” aliongeza.
LEAT ni mojawapo ya asasi za kiraia za kwanza kabisa nchini kupinga
ubinafsishaji wa migodi ya madini uliofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tatu na Nshala pamoja na aliyekuwa mwenzake katika taasisi hiyo, Tundu
Lissu (sasa mbunge), waliwahi kufunguliwa mashitaka na serikali kwa
sababu ya upinzani wao kwa sera hizo.
Kuhusu MIGA na ICSID
MIGA ni taasisi iliyo chini ya WB ambayo wawekezaji kutoka nchi
zilizoendelea huweka bima kwa miradi yao ya uwekezaji wanayoifanya
katika nchi masikini. Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1965.
Endapo nchi inayoendelea kama Tanzania itavunja mkataba wake na kampuni
hiyo, kampuni hiyo hupeleka kesi yake katika Mahakama ya Usuluhishi wa
Migogoro ya Kiwekezaji (ICSID) na kama itashinda MIGA italipa fedha
ambazo kampuni hiyo itadai kupoteza kutokana na uvunjwaji huo wa
mkataba.
MIGA ikishalipa, kazi yake itakuwa ni kufuatilia kuona nchi husika
inalipa fedha hizo na taasisi hiyo ina uwezo wa kukamata hata mali za
nchi husika ilimradi nayo ilisaini mkataba wa kukubali MIGA.
Tags
Profesa Muhongo