BANDA MEDIA BLOG

No title

 

DKT. STERGOMENA TAX AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA POLAND NCHINI



Waziri wa mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha
wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Poland waje nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya uchumi wa bluu na madini.

Waziri

Tax ameyasema hayo, wakati akihutubia mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland. Mkutano huo ambao
uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Poland na Ubalozi wa Tanzania
nchini humo umefanyika katika Ofisi za Taasisi ya Uwekezaji na Biashara ya
Poland zilizopo jijini Warsaw.

Mhe. Dkt.
Tax amesema Serikali chini ya uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania
imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili
kuvutia wawekezaji wengi wenye tija na mitaji waje kuwekeza nchini.


Ameyataja
maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji kutoka Poland na sehemu nyingine duniani
kuwa ni pamoja  uchimbaji madini, uchumi
wa bluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vya sukari na nguo na
miundombinu.


Amesema
ili kuhakikisha wawekezaji wanaofika nchini wanafikia malengo yao, Serikali
inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo,
kuboresha upatikanaji wa viza na vibali mbalimbali lakini pia Serikali
inaboresha mikataba mbalimbali ili kuondokana na urasimu wote kwenye sekta hiyo
muhimu ya uwekezaji. Pia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo
Bandari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji. Huduma
zingine zinazoboreshwa ni kuwa na umeme wa uhakika ambapo hadi sasa ujenzi wa
Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115  na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea
nchini.

 

Amesema ziara
yake nchini Poland pamoja na mambo mengine inalenga kukuza baiashara na
uwekezaji kati ya nchini hizi mbili.

 

“Ninawakaribisha
wafanyabaiasha na wawekezaji kutoka Poland kuja Tanzania. Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Mhe. Rais Samia imejipanga kikamilifu kuwahudumia. Tunaendelea
siku hadi siku kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini”
alisema Dkt. Tax.

 

Amesema
mbali na maboresho hayo, Tanzania ni nchi sahihi kwa wawekezaji kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo amani, miundombinu ya kisasa ya barabara, reli,
bandari na soko la uhakika kupitia uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya za
kikanda za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na
Soko Huru la Biashara Barani Afrika (CFTA)

 

“Serikali
imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha
biashara  kwa kupitia upya   sheria, kanuni na taratibu za
biashara  na kuzifuta zile  ambazo zimethibitika  kuwa
zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”

 

Mhe.
Waziri  amesema kwa kuwa nchi ya Poland
imepiga hatua kubwa katika masuala mengi ikiwemo teknolojia ya usimamizi wa
maji, Tanzania ingefurahi kuona wawekezaji kutoka nchi hiyo wanawekeza kwenye
sekta hiyo kwa wingi.

 

Amesema
kuwa uchimbaji wa madini kama vile Tanzanite na mengine mengi, ni fursa
nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Poland wanakaribishwa
kuichangamkia hapa nchini.

 

Kwa
upande wake, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo, 
 Bw. Zbigniew Sokal alitumia fursa
hiyo kumweleza utayari wa Taasisi yake kushirikiana na Taasisi za Uwekezaji
nchini ikiwemo TIC na ZIPA ili kujiimarisha zaidi. Alisema tayari makampuni
kadhaa ya Poland yapo tayari kuwekeza nchini Tanzania.

 

Wakati wa
Mkutano huo Wawakilishi kutoka Kampuni 10 za Poland zinazojishughulisha na
masuala mbalimbali  ikiwemo utengenezaji
wa mitambo ya kilimo, uchimbaji visima virefu, usimamizi wa maji na utunzaji wa
mazingira, teknolojia mpya ya uchomeleaji vyuma na  umeme wa jua waliwasilisha mada kuhusu
Kampuni zao.

                                                       

Wakati
huhuo,
 Mhe. Waziri Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea Mradi
mkubwa wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera uliopo  katika mji wa Jozefow. Mradi huo wa aina yake
pamoja na mambo mengine hususanya majitaka kutoka majumbani na kuyatibu kwa
matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji miti na maua katika mji huo. Kadhalika
takangumu zingine hutayarishwa kitaalam na kuwa mbolea ya samadi kwa ajili ya
mazao hayo ya miti na maua.

 

Akizungumza kuhusu mradi huo, Rais wa
Kampuni hiyo, Bw. Stanslaw Zdanowicz amesema mradi huo ambao unaendeshwa
kisasa, pamoja na mambo mengine umesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za
uondoshaji majitaka majumbani kwao.

 

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Tax alishukuru
kupata fursa ya kutembelea Kampuni hiyo na kujionea teknolojia ya hali ya juu
ya usimamizi wa kisasa wa majitaka na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini
kuja kuwekeza pamoja na kutembelea vivutio vya utalii vya nchini ikiwemo
Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

 

Mhe.
Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17
hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha
ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

 

Katika
ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC),  Mamlaka ya Ukuzaji  Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala
wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC).







Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG