BANDA MEDIA BLOG

No title

 

MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO YAENDELEA KUSHIKA KASI NCHINI,WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUWASAIDIA WATOTO



Mwenyekiti wa bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali  nchini,Mwantum Mahiza akizungumza na waandishi wa habari katika kikao hicho cha wadau jijini Arusha leo.
Kaimu msajili wa NGO’s nchini ,Mussa Sang’anya akizungumza  na waandishi wa  habari kuhusu kikao hicho Leo jijini Arusha.



Mkurugenzi wa shirika la kutoa malezi kwa watoto  SOS Tanzania,David Mulongo akizungumza kwenye kikao hicho cha wadau wa  mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya utetezi kwa watoto kilichofanyika jijini Arusha.
………………………….
Julieth Laizer ,Arusha.
Matukio ya ukatili wa  kijinsia kwa watoto yanaendelea  kushika kasi kutokana na wazazi  wengi kutokuwa na muda na watoto  hali  inayowafanya  watoto  kujiingiza  kwenda mambo yasiyofaa na kufanyiwa ukatili zaidi.
Aidha hali ya ukatili wa watoto kwa sasa hivi inaelezwa kuwa mbaya na hiyo  ikichangiwa na wazazi wenyewe kutokuwa na muda na watoto hivyo watoto kukosa elimu  ya makuzi  yaliyobora  na hivyo kupeleka kufanyiwa ukatili .
Hayo yalisemwa Leo jijini Arusha na  Mwenyekiti wa bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini ,Mwantum Mahiza  wakati akizungumza  katika kikao maalumu cha wadau wanaojihusisha na masuala  ya watoto jijini Arusha .
Mahiza amesema kuwa, kwa sasa hivi watoto wetu hawapo salama kwani wanafanyiwa mambo ya ajabu na ya kutisha na wanaofanya  hivyo ni  ndugu  wa  karibu jambo ambalo linawafanya  watoto wakose  amani hata ya kukaa kwenye familia zao. 
Amesema kuwa,watoto wanafanyiwa  ukatili kwa kiwango kikubwa sana hivyo ni  jukumu  la wadau mbalimbali wanaojihusisha na maswala ya watoto kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika  kutoa  elimu  kwa jamii kuhusu makuzi na malezi na swala zima la maadili. 
” mifumo iliyopo  kuanzia ngazi za chini ikitumika vizuri itasaidia kuzuia maswala ya ukatili  wa kijinsia wanaofanyiwa watoto kwani  huko  ndiko  sehemu sahihi watoto wataweza kuripoti matukio wanayofanyiwa kwa urahisi  zaidi  na kuweza kuchukuliwa  hatua  za kisheria mapema .”amesema Mahiza. 
Aidha ametaka swala zima la ukatili wa  kijinsia kwa watoto kushirikishwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa  mila,viongozi wa  dini  katika ngazi zote ili kwa pamoja waweze kuongeza  nguvu kukemea na kudhibiti  matukio hayo kwani  hali ya watoto kwa sasa ni  mbaya na  ukatili umekuwa mkubwa sana.
Kwa upande wa  Kaimu Msajili  wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’S) ,Mussa Sang’anya   amesema kuwa,swala zima la ukatili  wa kijinsia kwa watoto bado ni changamoto  kubwa sana, hivyo nguvu zaidi inatakiwa  kuongezwa kwa mashirika na hata wadau mbalimbali  ili kwa pamoja kuweza kushirikiana  katika kukemea matukio hayo. 
“Leo tumekutana hapa na ni kikao kazi  cha pamoja kuhakikisha kila mmoja wetu anakuja na maazimio na mikakati ya kufanya katika kudhibiti  swala zima la ukatili  wa  kijinsia dhidi ya watoto wetu na sisi kama wizara  tutaendelea  kutoa miongozo mbalimbali kuhakikisha watoto wanakuwa salama kila wakati.”amesema .
Aidha ameyataka mashirika binafsi yanayotetea  haki za watoto kuwa na nia moja ya dhati katika kusaidia watoto kupata haki zao na kuhakikisha usalama wa mtoto  unaendelea kulindwa  ,na kuhakikisha rasilimali  zinazopatikana kwa ajili ya watoto zinasambaa nchi nzima ili wote wapate huduma .
Naye Mkurugenzi wa shirika la kutoa malezi kwa watoto  SOS Tanzania,David Mulongo amesema kuwa wao kama shirika  wamekuwa wakifanya maswala ya kutetea na kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto kwani swala la kusaidia watoto ni la kila mmoja wetu kuhakikisha wote kwa pamoja wanashirikiana kutokomeza ukatili wa  kijinsia ambao wamekuwa wakifanyiwa  watoto kwa kiwango kikubwa. 
“Kikao hiki kimeandaliwa na wizara kwa kushirikiana na  sisi shirika katika kuangalia namna ya kuweka mikakati itakayosaidia kuwaokoa  watoto hawa kwani watoto wapo katika hatari kubwa kutokana na ukatili wanaofanyiwa kuanzia majumbani,kwenye taasisi wanazopata huduma hali ambayo imesababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la watoto wa  mitaani.”amesema  Mulongo. 
 
Ameongeza kuwa,nchi yetu  ina sera nzuri  na  mfumo mzuri wa kiutawala pamoja  na  sheria nzuri ila  changamoto ni kwamba lazima wadau waangalie wajue katika nafasi waliyopewa wajengewe mazingira  ya kuona swala la kulinda haki ya watoto liwe ni wajibu wa kila mmoja  katika serikali jamii na hata asasi za kidini  na kuna haja ya kuwepo  kampeni ya kitaifa kuhakikisha kila mdau anajengewa  uwezo kama kukumbushwa wajibu  kuwa swala la  kumlinda mtoto ni wajibu wa kila mmoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG