BANDA MEDIA BLOG

No title

 

TAMKO LA KAMATI YA SERA YA FEDHA



Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ilifanya kikao chake cha 229 tarehe 18 Desemba 2023,   Fax No. 2234217 

kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi. Katika tathmini yake, Kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha, umechangia kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki  ndani ya lengo la asilimia 5, kuongeza uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja  na kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha. Utekelezaji huu, ukichagiwa na Sera thabiti ya bajeti na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na shughuli za utalii  umesaidia kupunguza uhaba wa fedha za kigeni nchini kwa mwezi Oktoba na Novemba 2023.  

Kamati pia ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia na kubaini kuwa uchumi wa dunia  umeendelea kubaki dhaifu kwa kipindi cha mwaka 2023, kutokana na migogoro ya kisiasa,  kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani na ongezeko la bei za nishati. Hata hivyo, hali hii inatarajiwa kuimarika mwaka 2024 kutegemeana na kupungua kwa bei za nishati na  matarajio ya kupungua kwa kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi zilizoendelea pamoja na  utatuzi wa migogoro ya kisiasa duniani. Kamati pia ilifanya tathmini ya kina ya mwenendo wa  uchumi wa ndani na kubaini kuwa; 

  1. Licha ya changamoto zinazotokana na mtikisiko wa kiuchumi duniani, mwenendo wa  uchumi wa ndani ulikuwa wa kuridhisha mwaka 2023, na unatarajiwa kuimarika zaidi  mwaka 2024, kutokana na utekelezaji wa sera zenye lengo la kuchochea uzalishaji nchini  pamoja na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi. Pato la Taifa kwa Tanzania Bara lilikua  kwa asilimia 5.4 na asilimia 5.2 kwa robo ya kwanza na ya pili ya 2023, mtawalia.  Kutokana na ukuaji huu pamoja na tathmini ya viashiria vya awali vya kiuchumi kwa nusu  ya pili ya mwaka 2023, ukuaji uchumi unatarajiwa kuwa juu ya makadirio ya asilimia 5 kwa  mwaka 2023. Uchumi wa Zanzibar pia uliendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa  shughuli za utalii na uwekezaji wa sekta binafsi. Kutokana na hayo, ukuaji wa pato la taifa  kwa Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 5 katika robo ya pili ya mwaka 2023 na unatarajiwa  kufikia asilimia 7.1 kwa mwaka 2023.  
  2. Mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umeendelea kubaki chini ya lengo la asilimia 5,  kufuatia utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, bajeti na za kimfumo. Mfumuko wa bei  ulipungua kufikia asilimia 3.2 kwa mwezi Novemba na Oktoba 2023 ukilinganisha na asilimia 3.3 iliyorekodiwa kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo hadi Septemba 2023  kutokana na kupungua kwa bei za chakula nchini. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa  

bei uliendelea kupungua kufikia asilimia 6.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.5 mwezi Septemba 2023 kutokana na kushuka kwa bei za chakula na bidhaa zisizo chakula.  Mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia chini ya lengo la muda wa kati la asilimia 5 kwa  Tanzania Bara na Zanzibar. 

iii. Kufuatia utekelezaji thabiti wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi, ukuaji wa ujazi wa fedha ulipungua mwezi Novemba 2023. Ukuaji wa ujazi  wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 13.8 mwezi Novemba 2023, ukilinganisha na asilimia 14.5 kwa mwezi Septemba 2023. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa  sekta binafsi ilipungua kufikia asilimia 18.3 mwezi Novemba 2023 ukilinganisha na asilimia  19.5 mwezi Septemba 2023. Hata hivyo, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa juu  ya makadirio ya ukuaji wa asilimia 16.4 kwa kipindi kinachoishia Desemba 2023. Aidha, kuongezeka kwa hamasa ya uwekezaji sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji  biashara nchini zinategemea kuendelea kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. 

Ukusanyaji wa mapato ya Serikali ulikuwa wa kuridhisha, ambapo katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2023/24, makusanyo yalifikia asilimia 96 ya lengo kwa Tanzania Bara, huku matumizi  yakiendelea kuendana na mapato. Kwa upande wa Zanzibar, ukusanyaji wa mapato  ulishabihiana na malengo yaliyowekwa.  

  1. Nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, iliimarika kidogo  kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na  shughuli za utalii. Kufuatia hali hii, nakisi ya urari wa biashara na uhamisho mali nje ya  nchi ilifikia dola milioni 3,265.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka dola milioni 4,990.1 kwa 

mwaka unaoishia Oktoba 2022. Kwa upande wa Zanzibar, nakisi ya urari wa biashara,  huduma na uhamisho mali nje ya nchi iliongezeka kufikia dola milioni 477.7 kutoka dola  milioni 362.8, kutokana na kupanda kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma  kutoka nje. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha ikiwa ni takriban dola  bilioni 5 kwa mwezi Novemba 2023, kiasi kinachotosha kuagiza bidhaa na huduma nje  ya nchi kwa kipindi kinachozidi miezi minne. Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola  ya Marekani iliipungua kwa asilimia 7.8 kwa mwaka, hali inayoakisi upungufu wa fedha za  kigeni nchini. Hata hivyo, akiba ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha. 

  1. Sekta ya fedha iliendelea kuwa thabiti. Sekta ya benki ilibaki imara ikiwa na mitaji ya  kutosha na ubora wa rasilimali za benki ukiongezeka, kiwango cha mikopo chechefu  kilipungua kufikia asilimia 5.3 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.2 mwezi Oktoba 2022.  

Kamati ya Sera ya fedha iliridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kukabiliana na  uhaba wa fedha za kigeni nchini, Vilevile, utekelezaji wa sera zenye lengo la kuongeza mauzo ya  bidhaa nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, unatarajiwa kuimarisha 

urari wa bidhaa, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, kuongeza akiba ya fedha za kigeni na  hivyo kupelekea utulivu wa thamani ya Shilingi. Kamati pia ilipongeza jitihada zilizochukuliwa na  kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya programu mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwa ni pamoja na  yale yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF ya Extended Credit Facility (ECF).  

Vilevile, Kamati ilibaini na kupongeza hatua zillizofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika  kuhamia kwenye mfumo mpya wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha utakaoanza Januari 2024.  Utekelezaji huu utalenga riba za muda mfupi katika soko la fedha badala ya fedha taslimu  (reserve money) katika kukabiliana na mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa shughuli  za kiuchumi. Mfumo huu unatambulika kama Mfumo wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha  unaotumia riba.  

Kwa kuzingatia matarajio ya utulivu katika mfumuko wa bei na kuendelea kuimarika kwa  mazingira ya biashara nchini, Kamati iliridhia kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha  inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi mwezi Desemba 2023. Maamuzi  haya yalizingatia mwenendo usioridhisha katika uchumi wa dunia.  

GAVANA 

BENKI KUU YA TANZANIA

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG