Uchaguzi DRC 2023: Wananchi wajitokeza kupiga kura
Baadhi wa wakazi wa Kinshasa waliojitokeza mapema kupiga kura. Zaidi ya raia milioni 40 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanapiga kura nchini humo kuchagua viongozi wao. Picha/TRT Afrika.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya taifa la DRC mapema hii leo, wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura ambapo zoezi hilo limeanza saa kumi na mbili asubuhi. Zaidi ya wapiga kura milioni 40 watatumia nafasi hii leo kuchagua viongozi wao kuanzia ngazi ya urais, ubunge na madiwani.
Kuna jumla ya wagombea urais 26, huku rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi akiwania muhula wa pili. Katika uchaguzi huu, Tshisekedi anatoana jasho na wapinzani wake wakuu ambao ni Martin Fayulu, aliyekuwa waziri mkuu wa zamani.
Vile vile mmiliki wa TP Mazembe, klabu kongwe ya mpira wa miguu maarufu na yenye mafanikio makubwa kwenye historia ya soka nchini DRC na Afrika kwa ujumla, Moise Katumbi anategemea kutumia uzoefu wake wa uongozi kama Gavana wa Katanga.
Katika majimbo 26, yatakayopigiwa kura, Kinshasa ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya wapiga kura ambao wanafikia 5, 062, 991. Huku wastani wa majimbo mengine ukibaki kuwa ni wapiga kura milioni 1.3 kwa kila jimbo.
Kwa mara nyengine, uchaguzi wa mwaka huu pia umevutia mgombea mwanamke katika nafasi ya urais.
Marie Josee Ifoku (58) maarufu, ‘‘Mama wa fagio’’ hii ni mara yake ya pili kushiriki uchaguzi kama mgombea wa urais. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2018. Ifoku anaweka wazi uwezo wake na tajiriba aliyoipata mwaka 2018 kuwa imemfunza na itamsaidia kushinda mwaka huu.
Wakati huo huo, DRC imetangaza kufunga mipaka yake siku ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu DGM, ndege za ndani zimesitishwa, isipokuwa ndege za kimataifa katika viwanja vya ndege vya kimataifa.
